Wadau wa facebook

Maelezo

Kwa matukio na matangazo wasiliana nasi Simu no' {301}728-3977. Email:swahilivilla@gmail.com

Monday, August 30, 2010

AJALI MBAYA YAUWA WATU MABIBO DAR ES SALAAM

Watu wanne wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa katika ajali mbaya ya gari lililoacha njia na kugonga watu waliokuwa pembeni eneo la Mabibo mwisho jijini Dar es Salaam.

Gari hilo aina ya Toyota Surf lilokuwa likitokea maeneo ya Manzese liliacha njia na kugonga kibanda cha kuuza viazi vya kukaanga (chips) kilichokuwa na wateja mbalimbali na kisha kugonga ukuta wa duka na kuingia hadi ndani ya nyumba. Kamanda wa Polisi wilaya ya Kinondoni, Elias Kalinga alisema kuwa katika tukio hilo watu wanne walifariki dunia wakati wakipelekwa hospitali.

“Nimepata taarifa hizo sasa hivi nilikuwa Kijichi kwenye msiba wa askari mwenzetu. Waliokufa ni wanne, lakini hali ya wengine wengine 9 si nzuri na wamelazwa hospitali,” alisema Kalinga na kuongeza, “Kati ya majeruhi 9, saba wamelazwa Hospitali ya Muhimbili na wawili wamelazwa katika Hospitali Mwananyamala.”
Alisema kuwa dereva wa gari lililowagonga watu hao alitoweka mara baada ya ajali hiyo na alikuwa hajapatikana hadi jana jioni.

“Chanzo ni mwendo kasi. Nimeelezwa kuwa dereva alikuwa kwenye mwendo mkali na katika kujaribu za kukata kona alishindwa kumudu na kusababisha gari hilo kuvamia kibanda ambacho kilikuwa pembeni ya barabara hiyo,” alisema Kalinga.

Mashuhuda wa ajali hiyo walilieleza Mwananchi kuwa waliona watu saba wakiwa wameshapoteza maisha katika ajali hiyo iliyosababisha vurumai eneo hilo.

Mmoja wa mashahuda hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kuwa mtengeneza baiskeli ambaye hufanya shughuli zake mbele ya kibanda cha chipsi na duka, alikatika shingo na kufia papo hapo.

“Inatisha... ni ajali mbaya kwa kuwa mtengeneza baiskeli na watu wengine kama wane wamefia hapa hapa na ukijumlisha na wengine wanaweze kuwa tisa ambao wako hoi,” alieleza.

No comments:

Post a Comment