Wadau wa facebook

Maelezo

Kwa matukio na matangazo wasiliana nasi Simu no' {301}728-3977. Email:swahilivilla@gmail.com

Wednesday, September 19, 2012

Vurugu za Delta ya Mto Tana zimetoa changamoto mpya za usalama kwa Kenya

Utulivu hafifu umerejea katika eneo la Delta ya Mto Tana lililoko katika Jimbo la Pwani la Kenya kufuatia vurugu mbaya sana za kijamii zinazozuka katika eneo hilo kwa miaka.

Mwanaume wa kabila la Orma akiwa amepigwa picha kwenye kambi ya Shirika la Msalaba Mwekundu huko Delta ya Mto Tana tarehe 12 Septemba. Serikali ya Kenya ilitekeleza amri ya kutotembea usiku kuzuia vurugu katika eneo hilo. [Carl de Souza/AFP]

Kwa kipindi cha chini ya miezi miwili, mapigano ya kikabila kati ya makabila ya Pokomo na Orma yamegharimu maisha ya watu 110, wakiwemo askari polisi tisa, na maelfu ya familia kupoteza makazi. Mali zimeharibiwa na mifugo imeibiwa.

Rais Mwai Kibaki ametangaza kuweka amri ya kutotembea usiku katika maeneo hayo kama jaribio la kuzuia vurugu hizo.

Lakini vurugu mpya zilianza Jumapili jioni na mapema Jumatatu (tarehe 17 Septemba), ambapo si chini ya nyumba 20 ziliingiliwa katika vijiji vyote viwili, kwa mujibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Kenya. Siku ya Jumatatu, kaburi la halaiki liligunduliwa huko eneo la Garsen, eneo la mauaji ya hivi karibuni. Polisi wanatafuta amri ya mahakama kufukua miili hiyo ili kutambua utambulisho wao.

"Hali katika eneo la tukio bado ni ya kutia wasiwasi. Sijui ni nani wa kulaumiwa kwa vitendo hivi vya kutisha," Haro Daud, wa kabila la Pokomo, aliiambia Sabahi kwa njia ya simu. "Serikali lazima ichukue hatua kukomesha upotevu zaidi wa maisha,"

Joseph Karima, anayesimamia Delta ya Mto Tana kwa ajili ya Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya, alisema wanakijiji zaidi ya 13,700 wameathiriwa na vurugu, na wengi wamechagua kuhamishwa. Wengi wa wale wanaokimbia wanakaa katika makambi ya muda yaliyowekwa katika shule huko Tarasaa, Marereni, Garsen, Hola, Witu na Malindi, gazeti la Daily Nation la Kenya liliripoti.


Migogoro siyo mipya miongoni mwa wakulima Wapokomo, ambao wanalima kandokando ya Mto Tana, na wafugaji Waorma, ambao wanyama wao wanakunywa maji katika mto huo. Kwa miaka mingi, Wapokomo wamekuwa wakilalamika kwamba wanyama wanaomilikiwa na Waorma wanaharibu mazao yao. Vivyo hivyo, Waorma wanawalaumu majirani zao kwa kuziba njia ya kwenda mtoni.

Katika kambi ya muda ya Wapokomo wasio na makazi karibu na kijiji cha Semikaro, baadhi ya wakazi wanazilaumu siasa kwa usumbufu, wakidai walilengwa kwa ajili ya kufukuzwa kwa sababu ya uanachama wao katika Baraza la Jamhuri ya Kenya (MRC), kikundi kinachotaka kujitenga cha Mkoa wa Pwani ambacho kinatetea kugomea uchaguzi mkuu mwezi wa Machi ujao.

"Nafikiri wanasiasa, hususani wagombea wa ugavana na useneta, wanapanga njama za kufukuza kwetu kwa sababu ya uhusiano wetu na MRC," alisema Rova, ambaye anaishi katika kambi ya muda ya Semikaro, aliliambia gazeti la The Standard la Kenya. "Jambo hili ndilo linalotufanya tuamini kuna njama za kisiasa na huenda kuna mkono wa serikali katika uvamizi dhidi ya jamii."

Huenda kwa kushituliwa na ukubwa wa vurugu, baraza la mawaziri la Kenya, likiongozwa na Rais Mwai Kibaki, siku ya Alhamisi (tarehe 13 Septemba) liliiagiza polisi kutumia nguvu na kufanya uamuzi imara ili kumaliza mapigano. Naibu msemaji wa polisi Charles Owino amesema kimsingi polisi hawakutaka kutumia nguvu katika eneo hilo na kuchagua kufanya kwa tahadhari, wakisubiri idhini ya baraza la mawaziri.

Baraza la mawaziri liliidhinisha hatua kali za kurejesha amani katika eneo lenye vurugu, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa maofisa usalama 1,500 wa ziada.

Baraza la mawaziri pia liliagiza kuundwa kwa tume ya uchunguzi ya kimahakama, ambayo ina siku 30 za kuchunguza mapigano na kuwasilisha ripoti.

Koigi wa Wamwere, mbunge wa zamani kutoka Subukia katika Jimbo la Bonde la Ufa la Kenya, anasema mwitiko wa serikali umekuwa taratibu sana. "Inatangaza amri ya kutotembea muda fulani kuwa sio jambo la kufunga utulivu baada ya farasi kuchungwa?" aliandika tarehe 15 Septemba katika gazeti la The Star la Kenya. "Ukimya wa raisi katika mauaji ya kinyama ya watu wasiokuwa na hatia haukuanzisha njia ya, na kuhamasisha mauaji ya pili?"

Watu tisa wamekamatwa na kupelekwa mahakamani kujibu mashtaka kuhusu mapigano hayo, pamoja na Mtungaji sheria wa Galole Dhadho Godhana. Alishitakiwa siku ya Jumatano kwa kuchochea vurugu, ambazo alikanusha.

Majeshi ya usalama yajisambaza
Mauaji katika Delta ya Mto Tana yamesababisha changamoto mpya ya usalama kwa serikali ya Kenya, ambayo imetuma majeshi Somalia kupigana na al-Shabaab. Polisi wa Kenya pia wameongeza usalama wa ndani, kwani al-Shabaab walianzisha mashambulio kadhaa ya makombora huko Nairobi na Mombasa tangu mwezi Oktoba mwaka jana.

Siku ya Ijumaa, polisi walitoa tahadhari mpya ya ugaidi wakisema watuhumiwa nane walikamatwa na walipanga kufanya mashambulio ya mauaji nchini. Angalizo la mwisho lilitolewa baada ya kukamatwa kwa wanaume wawili huko Nairobi siku ya Ijumaa, mmoja alikubali kwamba ni mwanamgambo wa al-Shabaab. Wakati wa kukamatwa, maofisa walipata maficho ya baruti, pamoja na vizibao nane vya baruti, mabomu 12 ya kurushwa kwa mkono, bunduki nne za aina ya AK-47, mizunguko 480 ya risasi na mabomu mawili ya kutengenezwa.

Vurugu katika Delta ya Mto Tana zimetokea pia wakati nchi inajiandaa kufanya uchaguzi wake mkuu mwezi Machi, uchaguzi wa kwanza chini ya katiba mpya. Kenya ilishuhudia mawimbi ya vurugu wakati wa uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2007 zilizotokana na mabishano ya matokeo ya uchaguzi. Vurugu za uchaguzi uliopita zilisababisha watu 1300 kuuawa na wengine 600,000 kukosa mahali pa kuishi pamoja na kuharibika kwa mali zenye thamani ya mabilioni ya shilingi.

"Hali ya huko Mto Tana inasikitika sana," George Mathu, mkazi wa Eldoret, ambaye aliumizwa vibaya na vurugu za uchaguzi uliopita, aliiambia Sabahi. "Tunaamini mfumo wa usalama wa serikali utakuwa katika tahadhari kamili kuhakikisha matukio ya mabaya yaliyotokea mwaka 2007-2008 hayajirudii tena."

No comments:

Post a Comment