If you need it, we can provide: • USA 24 hours Passport service • Rush and emergency USA passport • Expedited Visa process for U.S. & foreign countries • Document Authentication •Document Legalization..For more information please contact us at: 703-286-7713

http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.htmlKwa kuchangia chochote kile alichonacho kupitia Hilmy Disability Charity Organisation. Wasiliana na Mkurugezi wa Hilmy Disability Charity Organisation. Faria Zam. kwa UK Number ya Simu. 745-501-4372 Au Abou Shatry. U.S.A No' 301-728-3977

 http://www.dickysmallsauto.com/

DICK SMALLS AUTO MOTIVE WE CAN HANDLE ALL OF YOUR REPAIR AND SERVICE NEEDS INCLUDING CALL US NOW!(301) 931-3300. 10111B BACOCON DRIVE,BELTSVILLE,MD 20705

Sunday, March 26, 2017

KENYA: JUBILEE ILIVYOMKUZA KISIASA 'SULTAN' JOHO

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wa Jubilee katika kaunti ya Mombasa kumshambulia na kumhangaisha Gavana Hassan Joho ina hatari ya kumkuza zaidi kisiasa naibu kiongozi huyo wa chama cha ODM, wadadisi wanaonya.

Ali Hassan Joho
GAVANA wa Mombasa, Ali Hassan Joho awahutubia wafuasi wake mjini Mombasa baada ya kurejea nchini kutoka Amerika Machi 5, 2017.

Wanasema, hii imedhihirika katika kura ya maoni ya hivi majuzi iliyoonyesha kwamba, wakazi wengi wa Mombasa watamchagua tena Bw Joho kuwa gavana wao.

Utafiti wa shirika la Tifa (Trend and Insights for Afrika) ulionyesha, Gavana Joho angehifadhi wadhifa wake iwapo uchaguzi mkuu ungeandaliwa leo.

Kulingana na utafiti huo, umaarufu wa Joho ni asilimia 68 dhidi ya asilimia 15 za mpinzani wake mkuu, Suleiman Shahbal wa Jubilee. Seneta Hassan Omar ni wa tatu kwa asilimia saba, akifuatwa na mbunge wa Nyali Hezron Awiti ambaye umaarufu wake ni asilimia tatu peke.

“Kwa kumhangaisha Gavana Joho ambaye anapendwa sana na wakazi wa Mombasa na eneo la pwani kwa jumla, Jubilee imemjenga zaidi. Kwa maoni yangu, hatua ya kumshambulia Bw Joho hadharani ilimkuza kisiasa na kumfanya sultan halisi,” asema Bw Joseph Waigwa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Alisema Serikali haingemzuia Bw Joho kuhudhuria hafla ya kuzindua feri ya Mtongwe iliyoongozwa na Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto.

“Wakazi wa Mombasa wanahisi kwamba, hatua hii ilionyesha Serikali ilihofia Joho angefichua mengi ambayo wameficha kuhusu miradi ya Serikali kuu eneo la pwani kwa jumla. Haukuwa uamuzi wa hekima kumzuia Bw Joho na kumfungia katika ofisi yake ilhali ni gavana aliyechaguliwa na wakazi wa Mombasa,” alisema.


Kunyoroshwa

Katika hafla hiyo, Rais Kenyatta alimlaumu Gavana Joho kwa kumfuata kila wakati akienda kufungua miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali kuu na kumtaka kuwaonyesha wakazi wa Mombasa alivyotumia pesa zinazotengewa kaunti yake.

Rais alimuonya Bw Joho kwamba, atamnyorosha akiendelea kumfuata, matamshi ambayo hayakupokelewa vyema na wafuasi wa Joho.

“Licha ya Serikali kumhangaisha, umaarufu wa Joho unazidi kuongezeka Mombasa na Pwani kwa jumla. Ukweli wa mambo ni kuwa, hatua ya Serikali ya kumhangaisha haijamuathiri kwa vyovyote,” asema Bw Waigwa ambaye ni mkazi wa Mombasa.

Anatoa mfano wa mikutano ya hadhara ambayo Bw Joho na magavana Amason Kingi (Kilifi) na John Mruttu( Taita Taveta) walifanya katika kaunti za pwani baada ziara ya hivi majuzi ya Rais Kenyatta pwani.

“Kumshambulia Gavana Joho hakukubadilisha ukweli kwamba, anatetea maslahi ya wakazi wa pwani ambao wanahisi wamekuwa wakidhulumiwa na Serikali. Rais angewapa suluhu ya matatizo yao badala ya kumshambulia Bw Joho,” asema Bw Seif Mwanjala, mdadisi wa siasa za eneo la pwani.

Uchunguzi

Katika kile kilichoonekana kuwa hatua ya kutimiza ahadi ya Rais ya kumhangaisha Gavana Joho, Serikali ilianza kuchunguza akaunti zake za benki, jambo ambalo gavana huyo alisema halimtishi.

“Nimepokea simu kutoka kwa moja ya benki ambazo mimi huweka pesa zangu. Wanasema eti wameagizwa na KRA kuchunguza taarifa kuhusu akaunti zangu tangu 2011 hadi leo.

Mimi niko na akaunti tatu kwenye benki za DTB, Stanbic na Barclays,” akasema Bw Joho.
Aliongeza kwamba, nia ya Serikali ni kutaka kumfilisi ili asiwe na nguvu za kifedha kushiriki katika siasa.

“Badala ya Serikali kutapatapa wakitaka kuchunguza, ninawashauri waende moja kwa moja kwenye benki hizo na kutwaa fedha zangu zote.

Mimi sikuzaliwa na fedha wala magari. Niko tayari kupoteza vyote ikiwa kufichua ufisadi na maovu Serikalini kutapelekea hayo yote. Sitanyamaza wala kutishwa,” akasema Bw Joho.

Kulingana na Bw Mwanjala, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba, imemzima Bw Joho kwa kusimama kidete kuipinga na kuikosoa.
Kibaraka

“Viongozi wa Jubilee wanataka kuweka gavana ambaye ni kibaraka wao ili kutimiza maslahi yao ya kibinafsi na sio ya watu wa Mombasa na pwani kwa jumla.

Wakazi wa pwani wanafahamu lengo hilo na hawako tayari kukubali kuwekewa viongozi na ndio sababu wameapa kumuunga Bw Joho ambaye anaonekana kutetea maslahi yao,” akaeleza Bw Mwanjala.

Akiongea akiwa kaunti ya Lamu wiki jana, Bw Joho alisema alikosana na Rais Kenyatta kwa kutetea maslahi ya maskwota eneo la pwani hasa walio katika shamba la ekari 900 linalobishaniwa la Waitiki.

“Uhasama wangu na Rais ulianza nilipouliza kwa nini maskwota wa shamba la Waitiki walitakiwa kulipa ada kabla ya kupatiwa vyeti vya kumiliki ploti walizopewa. Aliniambia ni kwa sababu wakazi wa pwani hawakumpigia kura,” Bw Joho alisema.

Baada ya tukio hilo, Serikali ilimpokonya walinzi na silaha katika kile wadadisi wanasema ilikuwa mbinu ya kumtisha lakini alisimama imara. “Mimi ninalindwa na Mungu. Wakae na walinzi wao,” alisema.

“Serikali pia imekuwa ikiwaandama jamaa zake wa karibu na kuchunguza kampuni zinazohusishwa na familia yake. Kufikia sasa hawajapata chochote cha kumpaka matope nacho jambo ambalo kwa wakazi wa Mombasa ni kumhangaisha gavana wao,” akasema.

Kumekuwa na madai kwamba Bw Joho anashiriki biashara ya dawa za kulevya ambayo amekanusha vikali.

Ripoti ilidai anasakwa na Amerika kwa kuhusika na biashara ya mihadharati. Lakini alizuru nchi hiyo kwa wiki mbili na kupokelewa kishujaa.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako