If you need it, we can provide: • USA 24 hours Passport service • Rush and emergency USA passport • Expedited Visa process for U.S. & foreign countries • Document Authentication •Document Legalization..For more information please contact us at: 703-286-7713

http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.htmlKwa kuchangia chochote kile alichonacho kupitia Hilmy Disability Charity Organisation. Wasiliana na Mkurugezi wa Hilmy Disability Charity Organisation. Faria Zam. kwa UK Number ya Simu. 745-501-4372 Au Abou Shatry. U.S.A No' 301-728-3977

 http://www.dickysmallsauto.com/

DICK SMALLS AUTO MOTIVE WE CAN HANDLE ALL OF YOUR REPAIR AND SERVICE NEEDS INCLUDING CALL US NOW!(301) 931-3300. 10111B BACOCON DRIVE,BELTSVILLE,MD 20705


Wednesday, April 19, 2017

Upande unaomuunga Lipumba wakimbilia mahakamani kuushtaki Benki ya NMB.

MGOGORO wa uongozi ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF) umezidi kukolea baada ya upande unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Ibrahim Lipumba, nao kuamua kukimbilia mahakamani kuushtaki uongozi wa juu ya Benki ya NMB.

MBUNGE WA MTWARA MJINI, MAFTAHA NACHUMA.

Uamuzi huo wa kukimbilia mahakamani umetokana na kile kinachodaiwa uongozi wa juu wa benki hiyo kukubali ombi la Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, kuzifunga kwa muda akaunti zote za chama hicho.

Oktoba mwaka jana Bodi ya Wadhamini ya CUF ilifungua kesi Mahakama Kuu dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Prof. Lipumba kwa kukiuka sheria ya vyama vya siasa.

Siku chache baada ya kutinga mahakamani kuwashtaki wawili hao, Maalim Seif alikiri kuziandikia barua benki zote zenye akaunti za CUF kuziomba kuzifunga hadi pale mgogoro ndani ya chama hicho utakapotatuliwa kutokana na kile alichokiita njama za Msajili kuupatia fedha za ruzuku upande unaomuunga mkono Prof. Lipumba.

Katika mahojiano na Nipashe kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa mwishoni mwa wiki, Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma ambaye anamuunga mkono Prof. Lipumba, alifichua mpango wa upande wao kwenda mahakamani kuushtaki uongozi wa juu wa Benki ya NMB.

"Kesi kubwa itakuwa Dar es Salaam ambayo tutamshtaki 'MD' (Mkurugenzi Mtendaji) wa NMB, lakini kutakuwa na kesi nyingine kwenye maeneo yote nchini ambako akaunti za CUF wilaya zimefungwa na mameneja wa benki hiyo," alisema mbunge huyo.


"Tunajaribu kusaka mwafaka, lakini kama majadiliano haya tunayoyafanya kwa sasa yatashindikana, maana yake tutakwenda mahakamani hivi karibuni kusaka haki yetu.

"Tulichobaini ni kwamba Maalim Seif alimwandikia barua 'MD' wa NMB akimwambia afungie akaunti zote za CUF wilayani. 'MD' akatuma nakala katika kila wilaya kwamba; akaunti zote za CUF za wilaya zifungwe. Tunachokijua sisi akaunti za CUF wilaya zimefunguliwa na wajumbe wa kamati tendaji ngazi ya wilaya."

Alisema akaunti za CUF wilaya wanazitumia kuweka pesa za michango ya wanachama na hivyo kufungwa kwake kutakiathiri kwa kiasi kikubwa chama kiuchumi.

"Kwa kifupi, akaunti hizi si kwa ajili ya ruzuku tu. Amezifunga karibu miezi minne sasa bila sababu yoyote ya msingi bali kwa kufuata maagizo ya mtu mmoja. Tunakwenda mahakamani hivi karibuni kusaka haki yetu," alisema.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya mbunge huyo na Nipashe.

SWALI: Ugomvi wa ruzuku ndiyo chanzo cha kusambaratika kwa vyama vikubwa vya upinzani miaka ya nyuma, kwa maana ya TLP na NCCR Mageuzi. Ugonjwa huu sasa naona unaingia CUF. Kuna dawa ya hii changamoto?

MAFTAHA: Ninachokiona mimi ni ubinafsi wa viongozi kama ilivyo kwetu sisi, kiongozi mmoja anaona yeye ndiye mwenye chama.

CUF yetu mpaka tulipofikia hapa si kwa sababu ya ruzuku, yaani huu mgogoro haujasababishwa na ruzuku bali ubinafsi wa baadhi ya viongozi wetu. Nafikiri ifike kipindi tuache kumwamini mtu, tuamini chama.

Ruzuku iliyoingia tukaipeleka kwenye wilaya (zaidi ya Sh. milioni 300) ilitoka kisheria na kwa kuzingatia taratibu zote cha chama. Tuliigawa hiyo ruzuu kwenye wilaya kwa sababu tangu Juni 2016, ruzuku ilikuwa haijapelekwa kwenye wilaya na kusababisha mambo mengi kukwama ikiwa ni pamoja na kutolipa kodi ya pango kwa ofisi zetu za wilaya na kutolipa watumishi.

SWALI: Kwa kumbukumbu zako, kipi hasa ndicho chanzo cha mgogoro uliopo CUF na kipi ambacho kingeweza kufanyika siku hiyo kuuepesha?

MAFTAHA: Kumbukumbu zangu, jinsi ninavyofahamu mgogoro ulianza hasa baada Mwenyekiti wa Chama, Prof. Lipumba alipoamua 'ku-resign' (kujiuzulu) uenyekiti kwa sababu za madhira ambayo alikuwa anafanyiwa na Katibu Mkuu. Hiki ndicho chanzo kikubwa. Kuna wakati Katibu Mkuu alikuwa anamfanyia madhira makubwa mwenyekiti na kubwa zaidi alikuwa anamzunguka mwenyekiti kwenye mambo mengi sana.

Na bahati nzuri kwamba CUF wakati ule tulikuwa tumekubaliana kuwekeza nguvu pande zote mbili za Muuungano wetu kwa maana ya Zanzibar na Tanzania Bara, kwa maaana kote kuwe na mtandao mmoja na mkubwa. Bahati mbaya ni kwamba Katiba ya chama imempa mamlaka Katibu Mkuu kuwa mtendaji mkuu wa mambo ya kifedha. Akawa anapeleka fedha nyingi Zanzibar.

Hata kwenye ule uchaguzi wa 2015, Zanzibar licha ya kuwa na 'population' (idadi ya watu) ndogo ya watu kama milioni moja na nusu, Tanzania Bara huku tuko zaidi ya milioni 45 na hapa ninaamanisha watu wote bila kujali hawa ni CCM, Chadema au NCCR Mageuzi, maana yake ukisema CUF tunakuwa wachache zaidi, 'resources' (nyenzo) zote za chama na maandalizi yote ya chama Katibu Mkuu anapeleka Zanzibar.

Kwa mfano, Juni 2015, Prof. Lipumba alishuhudia kwenye vyombo vya habari anazindua timu ya kampeni, kupeleka magari kila wilaya kwa ajili ya kampeni kule Zanzibar bila hata kumshirikisha mwenyekiti kwa sababu tu yeye ni 'Chief Accountant' (Mhasibu Mkuu) wa chama.

Mbaya zaidi, mwenyekiti akaona tu kwamba imepita kwenye karatasi Zanzibar imepelekewa Sh. milioni 600 kwa ajili ya maandalizi ya kampeni lakini huku Bara Sh. milioni 60 ambako ndiko kwenye watu wengi zaidi.

Mwenyekiti akawa anajitahidi kumweleza tukae pamoja tujadili kumbe Katibu Mkuu alikuwa na ajenda nyingine za siri ambazo mwenyewe anazijua. Kukawa na fitna miongoni mwa wakurugenzi wa chama, mkakati ambao ulifanikiwa kumwondoa Prof. Lipumba madarakani alipoamua mwenyewe kuachia ngazi.

Alipokuchukua uamuzi huo wa busara wa kujiuzulu, baadhi ya wanachama wa CUF wilaya wakaona chama kinayumba sana hasa katika nafasi ya uongozi.
Wakamshauri arudi kwenye chama na kumhakikishia kwamba wako nyuma yake.

Akaangalia katiba ya chama inasema nini, akaamua kurejea kwa sababu hapakuwa na taratibu zozote ndani ya chama zilizofanyika kuziba nafasi yake au kukubali kujiuzulu kwake na yaliyofuata kila mtu anayajua -- kuvurugika kwa mkutano pale Dar es Salaam na mambo mengine mengi.

Kwa hiyo, katika kujibu swali lako, hiki kingeepukika kama tu Katibu Mkuu angefuata Katiba ya CUF Ibara ya 117 na kuwasikiliza wajumbe wa mkutano mkuu kwa yale waliyokuwa wanataka. Kama alikuwa hamtaki Prof. Lipumba, angesubiri tu hadi mwaka 2019 kwa sababu CUF tuna uchaguzi mkuu wa chama. Prof. Lipumba angeachwa aendelee mpaka wakati wake ukifika maana kama watu hawamtaki, wanaweka mtu mwingine.

SWALI: Ukipata nafasi ya kukaa meza moja na Maalim Seif leo, utamshauri nini katika mazungumzo yenu?

MAFTAHA: Nitamshauri yale ambayo nilimweleza kwenye mkutano mkuu, na pia nilipokutana naye nyumbani kwake pale Ilala, Dar es Salaam. Nilishaenda nyumbani kwake, nikakaa naye saa nzima naongea naye kipindi mgogoro ulipoanza tu.

Nilimweleza kwamba, kimsingi kwa mujibu wa katiba hii ya CUF, Prof. Lipumba bado ni mwenyekiti halali wa chama. Kwa hiyo, kwa sasa tumuache, tufike 2019 huko tutakapofanya uchaguzi mwingine. Kama wanachama hawamtaki, tutambadilisha wakati huo.

Kubwa zaidi ni kwamba wakae pamoja na wajadiliane, suala la kwamba mimi simtaki Prof. Lipumba, simtaki mtu fulani, sijawahi kushindwa katika maamuzi yangu. Binadamu yeyote huwezi kusema hujawahi kushindwa, ni Mungu peke yake.

Mimi nikipata nafasi, nitamweleza haya haya tena; kwamba akae chini na mwenyekiti, aje ofisini Buguruni. Kama hamtaki, asubiri tufanye uchaguzi 2019, wajumbe watafanya uamuzi kwa sababu chama si cha mtu mmoja. CUF si ya Prof. Lipumba wala Maalim Seif, ni mali ya wanachama.

SWALI: Unafikiri CUF ya mwaka 2010 inaweza kurudi?

MAFTAHA: CUF ya mwaka 2010 ni CUF dhaifu kuliko ya CUF ya mwaka 2017. Hii ya mwaka huu wa 2017 iko juu sana na ninaamini hata wewe unaweza kukubaliana na hili. Miongoni mwa vyama ambavyo vinatajwa sana katika kipindi hiki, namba moja ni CUF.

Kutokana na mgogoro huu uliopo wa Maalim Seif kutomtaka Prof. Lipumba, CUF imetajwa, imetajwa kweli kweli kwenye maeneo mengi. Mwaka 2016 na 2017, hakuna chama cha siasa Tanzania ambacho kimetajwa kama CUF.

Kwa hiyo, chama chetu sasa hivi kinajulikana sana. Hata watu ambao walikuwa hawaijua CUF, sasa wameijua CUF, hivyo ni dhahiri kwamba CUF itaendelea kuwa juu, itaendelea kutajwa, itaendelea kuvuna wanachama wengi kwa sababu kila siku napigiwa simu kutoka maeneo mengi, watu wanataka kujiunga na CUF.

Mimi ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF Taifa. Kwa mara ya kwanza naona CUF tumepata 'coverage' (kusikika) kubwa kuliko miaka mingine yote. Kwa hiyo, niseme tu kwamba ninapoulinganisha mwaka 2010 na mwaka 2017, naona chama kwa sasa kinatajwa zaidi kuliko ilivyokuwa 2010 na hata mtandao wa chama umekuwa ni mkubwa zaidi kuliko ulivokuwa kipindi hicho.

Ni ukweli usiopingika kwamba CCM wako juu kwenye uwakilishi bungeni. Wako zaidi ya 200 wakifuatwa na Chadema ambao wako zaidi ya 70 na baadaye CUF ambao tuko 42.

Yalitokea mambo mengi CUF kuporomoka kutoka namba mbili hadi namba tatu kwa sababu CUF ni karibu awamu mbili imewahi kuongoza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tangu vyama vingi vilipoanza.

Tukisimamia sera yetu vizuri na kuyakwepa mambo ambayo yanawafanya Watanzania wakose furaha na kuifanya nchi yetu kuwa ya tatu kutoka mkiani kwa nchi ambazo wananchi wake hawana furaha, tukasimamia misingi ya utawala bora na demokrasia, tutafanikiwa kurejea katika nafasi yetu na hata kuongoza nchi. Tukiwa na mtandao mpana nchi nzima na kuacha kulalia upande mmoja wa Muungano, chama kitajieneza kwa sera yake ya 'Haki Sawa kwa Wote' na ahadi yetu ya utajilisho ya kuinua kipato cha wananchi bila ufisadi.

Ni imani yangu, mwaka 2019 CUF itachukua viti vingi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na 2020 itakuwa na madiwani na wabunge wengi kuliko hawa waliopo kwa sasa kwa sababu ya sera yetu ya utajilisho na Haki Sawa kwa Wote na kukemea ufisadi.

SWALI: Kitendo cha wabunge wenzenu wa CUF kutoka bungeni pale unapopata nafasi ya kuchangia, kinakuathiri vipi?

MAFTAHA: Suala la wabunge awa CUF kutoka ni kutekeleza maagizo ya waliowatuma kwenye vikao vyao na huyo wanayekutana naye. Walichoambiwa huko kwenye vikao vyao ni kututenga mimi na (Magdalena) Sakaya.

Wala sijali, kutoka kwao ni demokrasia. Lakini nashauri wanapoamua kutoka, waondoke kabisa na wasisaini posho za kuhudhuria vikao vya Bunge. Wapo wabunge wa CUF ambao hata salamu hawatoi kwetu. Nafikiri tumeshindwa kujitambua kama wabunge wa CUF.

Baadhi yetu tunaamini hatuwezi kushinda bila msaada wa vyama vingine. Mimi nilishindana na vyama vyote Mtwara na nikashinda. Ninasimamia kile ninachokiamini ni sahihi.

Naamini mambo haya hayatachukua muda mrefu, yatakwisha.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako