If you need it, we can provide: • USA 24 hours Passport service • Rush and emergency USA passport • Expedited Visa process for U.S. & foreign countries • Document Authentication •Document Legalization..For more information please contact us at: 703-286-7713

http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.htmlKwa kuchangia chochote kile alichonacho kupitia Hilmy Disability Charity Organisation. Wasiliana na Mkurugezi wa Hilmy Disability Charity Organisation. Faria Zam. kwa UK Number ya Simu. 745-501-4372 Au Abou Shatry. U.S.A No' 301-728-3977

 http://www.dickysmallsauto.com/

DICK SMALLS AUTO MOTIVE WE CAN HANDLE ALL OF YOUR REPAIR AND SERVICE NEEDS INCLUDING CALL US NOW!(301) 931-3300. 10111B BACOCON DRIVE,BELTSVILLE,MD 20705


Friday, July 14, 2017

RAILA AHIMIZA WAKENYA KUDUMISHA AMANI WAKATI WA KAMPENI

Na SAMMY WAWERU na LAWRENCE ONGARO

MUUNGANO wa upinzani National Super Alliance (NASA) ukiongozwa na kinara wake Raila Odinga Alhamisi uliendesha kampeni za kusaka kura katika baadhi ya maeneo ya Kaunti ya Kiambu na Murang'a.

Raila Odinga
Raila Odinga. Picha/LAWRENCE ONGARO

Kaunti hizi ni moja wapo wa zinazoaminika kuwa ngome kuu za Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia ndiye kinara wa mrengo wa Jubilee akisaidiwa na Naibu wake William Ruto.

Katika baadhi ya maeneo ya Kaunti ya Murang'a aliyozuru Bw Raila akiandamana na vinara wenza Musalia Mudavadi na Moses Wetang'ula, waliuza sera zao kwa amani huku wakionekana kushabikiwa na wananchi waliojitokeza. Safari iling'oa nanga Kennol, msafara wao ukaelekea Kakuzi, Kandara na maeneo mengine ambayo amani ilitawala hotuba zao.

Kitumbua kiliingia mchanga walipotua mjini Thika ambapo makundi mawili, kimoja cha Jubilee na kingine cha NASA, yalipokabiliana vikali na kulazimisha maafisa wa usalama kutumia vitoa machozi kutuliza ghasia hizo. Aidha kikundi kinachoshukiwa kuwa cha Jubilee kwa sare walizokuwa wamevalia kilizua rabsha kikikataa Raila na vinara wenza wahutubu Thika, huku kile cha NASA kikikabiliana nao vikali. Hotuba zao hazikukamilika na hawakuwa na budi ila kuchukua gari mguu niponye ili kukwepa ghadhabu za kikundi hicho.

Msafara huo ulipowasili Githurai 45, ulikaribishwa kwa shime. Vinara hao walipoanza kuhutubu moja baada ya mwingine, ghafla mandhari na taswira ikageuka na kuwa ya kuwarushia mawe. Maafisa wa usalama hawakuwa na budi ila kutumia vitoa machozi kutuliza rabsha hizo, nao vinara wakishurutika kusitisha mkutano wao na kutoweka.


Mtaa wa Githurai 45 na Mji wa Kiambu, yote ipo katika Kaunti ya Kiambu.

Kiongozi wa NASA Bw Raila Odinga, alisema matukio ya aina hiyo huwa yamepangwa na yanastahili kukomeshwa mara moja.
"Kila kiongozi anastahili kuzuru kila eneo la nchi hii bila kutatizwa na yeyote, na pia sisi kama viongozi tunastahili kujizuia," alisema Bw Odinga.

Alisema mbinu ya kutwaa vitambulisho vya wakongwe na serikali, kwa kisingizio cha kulipwa pesa za uzeeni unastahili kuchunguzwa kwa kina, huku akiishauru tume huru na mipaka ya IEBC ichunguze jambo hilo kwa makini.

"Tunaelewa vyema Wakenya wamechoka na wangetamani mabadiliko na ni vyema pia kulinda kura kwa vyovyote vile ili kusije kukawa na hali ya wizi wa kura," alisema Bw Odinga.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi jioni katika mahojiano ya moja kwa moja kwa kituo cha runinga cha NTV katika boma lake la Karen, Nairobi alipokuwa akihojiwa kuhusu masaibu yake alipokuzuru Mlima Kenya mnamo siku hiyo.

Alisema wamekuwa wakizungumzia mengi kuhusu IEBC ili waweze kuweka uwanja wa uchaguzi uwe mwema kwa kila kiongozi.
"Tume ya IEBC ndiyo itaweza kuokoa nchi hii kwa kuwapa wakenya uchaguzi ulio huru haki na uwazi. Kwa hivyo hatungependa kusikia visingizio hapo baadaye eti kulikuwa hivi na vile," alisema Bw Odinga.

Alisema rejista ya wapiga kura inastahili kusafishwa ili liwe na majina ya wapigaji kura halali bila kujaza walioaga dunia hapo awali.

Alisema iwapo NASA itapata uongozi itahakikisha ufisadi umevunjwa kabisa kwani hiyo ndiyo donda sugu linalofyonza uchumi wetu hapa nchini.

Hata hivyo kinara wa NASA mapema Ijumaa amekashifu matukio hayo akiyata kuwa ya kiupuzi na yaliyopitwa na wakati ikizingatiwa taifa hili lina uhuru wa demokrasia iliyopiganiwa mwaka wa 1992 na kuruhusu mfumo wa kuwepo kwa vyama vingi.

"Hayo ni maneno na mambo ya kusikitisha sana. Ni utoto, iwapo hutaki kusikiliza mtu usihudhurie mkutano wake. Hilo ni jambo la kiujinga lililopitwa na wakati," akaeleza Raila kwenye mahojiano na Radio Citizen kipindi cha Jambo Kenya.

Aidha amedokeza kuwa huenda vijana waliozua rabsha walikuwa wamelipwa na wapinzani wake ili kumharibia lengo la kuomba kura akihoji kuwa makaribisho kila walipoenda yalikuwa ya ukarimu na mambo yakawa yakienda segem nege pindi walipoanza kuhutubu.

"Naona hao vijana walikuwa wamelipwa kwa sababu walikuwa na sare za Jubilee. Hata hivyo nimewasamehe kwa kuwa mimi ndiye Baba yao," amesema.

Akaongeza: "Hao watu waliletwa pale kurusha mawe (akimaanisha Thika na Githurai 45). Sisi kama NASA tunalaani tukio hilo na tunashauri wafuasi wetu wasifanyie wapinzani wetu vitendo vya aibu kama hivyo."

Japo Swahilihub ambayo ilihudhuria mkutano huo Githurai 45 kwenye mahojiano ya kipekee na walioshuhudia rabsha hizo kuna waliohoji kuwa zilizushwa na walinzi wa vinara hao. "Mzozo huo ulitokea kwa sababu ya walinzi wao ambao walikuwa kiini chake, sisi tulikuwa radhi kumsikiliza," akaeleza mzee mmoja aliyeomba kubana jina lake.

Kuna waliokashifu tendo hilo wakisema si haki wala demokrasia. "Waliowarushia mawe hawakuonyesha demokrasia yoyote. Wanafaa wajue Raila Odinga ni moja wapo wa viongozi tajika waliotoa taifa hili maisha ya utumwa," akadokeza kijana aliyeomba pia kubana jina lake.

Waziri huyu Mkuu wa zamani ameeleza kuna haja ya kutilia maanani maana ya demokrasia. "Tunashauri wananchi kinara yeyote akiwatembelea wamsikilize na wadumishe amani. Iwapo hakufurahishi usihudhurie mkutano wake. Demokrasia ni: Usikilize ajenda zake kisha uamue ni nani utakayempigia kura," akakariri Raila.

"Sehemu ambazo nimezuru jimbo la Kati ikiwemo Karatina, Kennol, Nyeri mjini na Othaya wote huniita 'Mutongoria Njamba' (Kiongozi shupavu) zingine ni porojo za wapinzani wangu ati mimi ni 'Mundu muguruki' (Mwendawazimu)," akaongeza akisuta Jubilee.

Itakumbukwa kwamba taswira sawia na iliyoshuhudiwa Thika na Githurai 45, ilitokea katika maeneo ya Nyanza na Kaunti ya Baringo mnamo Jumatano Julai 12.

Aidha Naibu Rais William Ruto alizomewa na wananchi wa Kaunti ya Homabay wakidai wanataka kuhutubiwa na Rais Kenyatta. Kabarnet Kaunti ya Baringo, mkutano wa NASA ulilazimika kusitishwa ghafla kwa sababu wananchi walizua rabsha na kufurusha vinara wa muungano huu.

Wachanganuzi wa maswala ya kisiasa wanahoji iwapo mpiga kura haridhishwi na kiongozi fulani, basi asihudhurie mkutano wake au akihudhuria amruhusu ahutubu na adumishe amani.

"Iwapo hupendi wala kuridhishwa na mwanasiasa fulani, usihudhurie mkutano wake. Endapo utauhudhuria msikilize kwa utulivu na udumishe amani kisha utaamua ni nani utakayemchagua," amesema mwanaharakati Brian Weke ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga Ijumaa.

"Kuzomea wanasiasa ama kuwarushia mawe hiyo si demokrasia, hizo ni siasa za zamani zilizopitwa na wakati," akaongeza.

Kama ilivyo ada ya kila mwanasiasa, Raila hakukosa kuuza sera za muungano wake kwenye mahojiano hayo. Ameendele kukanusha madai ya Jubilee kuwa NASA haipo tayari kwa kupinga kila mkakati wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kwenye maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 8.

"Hizo ni porojo za Jubilee kwa sababu wanajua uchaguzi ukifanyika leo tutawashinda. Wanatumia IEBC, tumekuwa tukienda mahakamani ili kuondoa vikwazo vilivyoko na kushinda kesi zote kwa ajili tunataka uchaguzi wa huru, haki na uwazi," akasema.

Bw Wafula Chebukati ndiye mwenyekiti wa tume ya IEBC.

"Sisi kama NASA tuko tayari kushiriki uchaguzi hata ungefanyika jana. Tunataka ufanyike kisheria na sharti ufanyike Agosti 8 ndio maana sisi huhubiri nane nane. Hatutaki nusu mkate, tunataka ukiwa mzima na kamili," akaongeza akiuza sera za manifesto ya NASA hususan kubuni nafasi za ajira kwa vijana na kupunguza gharama ya maisha ambayo imepanda sana.

Kinara huyu amesema endapo atachaguliwa kuwa rais, serikali yake itaboresha uchumi kutoka asilimia 5 hadi 7 na hatimaye 10 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo, kisha ampokeze kinara mwenza Kalonzo Musyoka mwaka wa 2022 awanie urais.

Mrengo wa Jubilee kwenye kampeni zake umekuwa ukisuta vinara wa NASA kwamba walikuwa kwenye serikali za awali kwa zaidi ya miaka 20 na hakuna walichofanyia taifa hili.

Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto hujigamba kuwa miaka 4 tangu wachukue serikali mwaka wa 2013, wamefanya makuu na hata zaidi yaliyofaa kufanywa na vinara wa NASA walipokuwa serikalini.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako