If you need it, we can provide: • USA 24 hours Passport service • Rush and emergency USA passport • Expedited Visa process for U.S. & foreign countries • Document Authentication •Document Legalization..For more information please contact us at: 703-286-7713

http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.htmlKwa kuchangia chochote kile alichonacho kupitia Hilmy Disability Charity Organisation. Wasiliana na Mkurugezi wa Hilmy Disability Charity Organisation. Faria Zam. kwa UK Number ya Simu. 745-501-4372 Au Abou Shatry. U.S.A No' 301-728-3977

 http://www.dickysmallsauto.com/

DICK SMALLS AUTO MOTIVE WE CAN HANDLE ALL OF YOUR REPAIR AND SERVICE NEEDS INCLUDING CALL US NOW!(301) 931-3300. 10111B BACOCON DRIVE,BELTSVILLE,MD 20705

Thursday, August 30, 2018

NINI KINAWATAFUNA WAPIGAKURA WALIOANDIKISHWA TZ?

Na DANIEL MJEMA

KUNA jambo lisilo la kawaida ambalo limejitokeza katika chaguzi ndogo ambazo zimekwishafanyika, nalo ni mwitikio mdogo wa wapigakura kulinganisha na mwamko wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Foleni ya kupiga kura
Foleni ya wapigakura. Picha/MAKTABA

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, idadi ya wapigakura waliojitokeza ilikuwa kati ya asilimia 60 na 86 ya waliojiandikisha, lakini leo katika chaguzi ndogo baadhi ya maeneo wanajitokeza asilimia 17 tu.

Mathalan, katika uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni uliofanyika Februari, 2018, walioandikishwa kupiga kura ni 264,055 lakini waliopiga kura ni 45,454 ambayo ni sawa na asilimia 17 tu.

Katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Mawenzi katika Manispaa ya Moshi uliofanyika Agosti 12, 2018, waliojitokeza kupiga kura ni 565 sawa na asilimia 31.4 tu ya watu 1,800 waliojiandikisha.

Taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya uchaguzi mkuu wa 2015, inaonyesha, waliopiga kura walikuwa 15,596,110 sawa na asilimia 67.34 ya wapigakura walioandikishwa 22,658,247.

Takwimu hizi zina tafsiri moja tu. Kuna jambo haliko sawa ambalo linawatafuna wapigakura ambao katika kipindi kisichozidi miaka mitatu tu kuanzia 2016 kupiga kura kibao wameamua kususa.

Hakuna ubishi, wapo waliojiandikisha kupiga kura kwa lengo la kupata vitambulisho ili wavitumie kwa sababu mbalimbali ikiwamo kusajilia laini za simu na kudhamini ndugu mahakamani.

Ukisoma maandiko ya wasomi mbalimbali duniani, wanaeleza sababu mbalimbali zinazoweza kusababishia wananchi wasione umuhimu wa kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wowote ule.


Wapo ambao hawajali kupiga kura na inawezekana ni kutokana na kukosa taarifa, au uvivu; na wapo ambao hawana elimu ya uraia, hawaelewi vya kutosha juu ya Serikali, mchakato wa uchaguzi na sera za vyama vya siasa.

Si hivyo tu lakini wapo ambao wameaminishwa tu bila kuwapo ushahidi wa kisayansi kuwa hata wakienda kupiga kura, hawataweza kuleta mabadiliko kwa madai eti CCM wataiba kura.

Jeshi la Polisi nalo linanyooshewa kidole japo hakuna ushahidi, kuwa linatumika kulinda masilahi ya CCM katika chaguzi hizo badala ya kuteleza majukumu yao kwa weledi na haki.

Madai na tuhuma hizi hazijatolewa ufafanuzi wa kina na wa kutosha, mathalan katika Jimbo la Buyungu, mgombea wa Chadema, Eliah Michael ametoa madai mazito dhidi ya Tume.

Katika madai yake ambayo naamini hata NEC imeona video inayotembea mitandaoni, Michael anadai fomu za matokeo kutoka kwa mawakala wake ni tofauti kabisa na alizokuwa nazo msimamizi.

Tayari Marekani kupitia Ubalozi wake hapa nchini imeeleza kusikitishwa na uendeshaji wa chaguzi ndogo za ubunge huko Buyungu na katika kata mbalimbali nchini.

Taarifa hiyo ya Marekani ambayo imepingwa na NEC, ikilitaka taifa hilo kutoa ushahidi, imebainisha ukiukwaji wa haki na sheria za uchaguzi, vitisho vya polisi dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani na watu kukamatwa kiholela.

Taifa hilo limeenda mbali na kutahadharisha kuwa mambo haya yanakwaza haki ambazo Katiba imewapa raia wake na kuhatarisha amani, utulivu na usalama nchini na katika eneo lote la kanda.

Pengine tunapoelekea katika chaguzi za serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020, ni wakati mwafaka kwa NEC na vyombo vingine vinavyosimamia uchaguzi kujitafakari kwa kina.

Nani wa kuogopwa zaidi?

Huu ni wakati wa kufanya utafiti wa kina kujua sababu za wapigakura wengi tena baadhi ya maeneo wanafika hadi asilimia 60 hadi 80 hawajitokezi kupiga kura. Nini kinawatafuna?

Kiongozi wa Kijeshi wa Ufaransa (1811-1821), Napoleon Bonaparte aliwahi kusema “The people to fear are not those who disagree with you, but those who disagree with you and are too cowardly to let you know”.

Kwa tafsiri isiyo rasmi anasema, “Watu wa kuwahofia sio wanaotofautiana na wewe, bali wanaotofautiana na wewe na wakaogopa kukuambia.”

Tusijidanganye, mkusanyiko wa chuki unaojengeka kutokana na yanayojitokeza katika chaguzi hizi hauna afya kwa mustakabali wa amani na mshikamano wa taifa letu kama Marekani ilivyoonya.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako