If you need it, we can provide: • USA 24 hours Passport service • Rush and emergency USA passport • Expedited Visa process for U.S. & foreign countries • Document Authentication •Document Legalization..For more information please contact us at: 703-286-7713

http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.htmlKwa kuchangia chochote kile alichonacho kupitia Hilmy Disability Charity Organisation. Wasiliana na Mkurugezi wa Hilmy Disability Charity Organisation. Faria Zam. kwa UK Number ya Simu. 745-501-4372 Au Abou Shatry. U.S.A No' 301-728-3977

 http://www.dickysmallsauto.com/

DICK SMALLS AUTO MOTIVE WE CAN HANDLE ALL OF YOUR REPAIR AND SERVICE NEEDS INCLUDING CALL US NOW!(301) 931-3300. 10111B BACOCON DRIVE,BELTSVILLE,MD 20705

Friday, October 19, 2018

CHADEMA WALIMALIZA SUALA LA KUBENEA NA KOMU KIAINA

Na ELIZABETH EDWARD, DAR ES SALAAM, Tanzania

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetaja hatua nne ambazo kiliwachukulia wabunge wake, Saed Kubenea na Anthony Komu baada ya wawili hao kukiri kupanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

John Mnyika
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika (kushoto) akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari Oktoba 18, 2018, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa itifaki na mambo ya nje wa Chama hicho, John Mrema. Picha/ERICKY BONIPHACE

Uamuzi huo ni maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichoketi juzi katika Hoteli ya Bahari Beach kikiwa na ajenda moja tu ya kuwahoji wabunge hao. Walihojiwa kwa dakika 281.

Komu na Kubenea katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Alhamisi makao makuu ya chama hicho Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini hapa, waliomba radhi kwa mazungumzo yao dhidi ya Jacob yaliyosambaa katika mitandao ya kijamii.

Katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisoma maazimio ya Kamati Kuu na kubainisha kuwa wabunge hao wamepewa onyo kali, kutakiwa kuandika barua ya kuomba radhi kwa chama na waliotajwa katika mazungumzo yao.

Adhabu nyingine ni kuwekwa kwenye kipindi cha uangalizi kwa mwaka mmoja pamoja na kuvuliwa nafasi zao za uongozi ndani ya chama na kubaki na ubunge pekee, huku wakipewa nafasi ya kuzungumzia jambo hilo.

Kubenea na Komu katika siku za hivi karibuni walizua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa ni sauti yao kusikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Jacob, lakini kwa nyakati tofauti walikanusha kuwa ni ya kutengeneza huku Jacob akibainisha kupeleka suala hilo ndani ya chama.

Hata hivyo, Alhamisi walikiri kuwa sauti hizo ni zao na Kubenea akawa wa kwanza kuzungumza na kuomba radhi.


Kubenea aomba radhi

“Kama ambavyo mmeelezwa (na Mnyika) nichukue nafasi hii kusema kwamba yaliyotokea siku hiyo ni bahati mbaya na hatukuwa na nia yoyote ovu kwa msingi huo, naomba radhi wote walioguswa na Watanzania kwa jumla,” alisema Kubenea ambaye ni Mbunge wa Ubungo.

Alisema hana tatizo lolote na Jacob na amekuwa akifanya naye kazi kwa ushirikiano na ni rafiki yake wa karibu.

Alipoulizwa kuwa ana dalili za kuhama Chadema, Kubenea alisema, “Mimi ni imara mno ningekuwa legelege nisingeenda mbele ya Kamati Kuu. Uthibitisho wa kwenda mbele ya kamati kuu na kupita vigingi vyote hivyo ni wazi kuwa mimi ni imara na sina mpango wa kuihama Chadema. Waambieni CCM mimi ni imara hawaniwezi.”

Komu azungumzia ilivyokuwa

“Nichukue nafasi hii kwanza kukishukuru chama kwa jinsi kilivyolichukulia jambo hili na kulipa uzito. Chama ni kikubwa kuliko sisi wote na sisi ni vyombo vya chama,” alisema mbunge huyo wa Moshi Vijijini.

“Chama kina mikono yake. Kwa kutambua sisi ni vyombo vya chama tunatekeleza maagizo na tayari tumeshaandika barua za kuomba radhi.”

Teknolojia yawaumbua

Komu alikiri kusambaa kwa sauti hiyo kuwa ni matokeo ya wao kuumbuliwa na teknolojia, “Mazungumzo yangu na Kubenea yalikuwa ya faragha na yalianzia mbali ila teknolojia ilituzidi yakajirekodi na kujituma.”

“Ile clip (sauti) ilikwenda hewani kwa bahati mbaya mazungumzo yetu yalikuwa siri ila ndiyo hivyo teknolojia imetuzidi. Nilishika simu kwa bahati mbaya nikabonyeza cha kurekodia ndiyo ikaenda. Kwa mujibu wa katiba yetu kupeleka kitu chochote mtandaoni kinachohusu masuala ya chama ni makosa na hicho ndio tunachoombea radhi.”

Alisisitiza, “Unajua mnavyokuwa kwenye faragha mnajiachia. Kwa hayo yaliyotokea tunaomba radhi, tunataka kuanza ukurasa mpya bila kuwa na kigugumizi.”

“Tunataka kuanza ukurasa mpya bila kuwa na kigugumizi. Tunatoka hapa tukiwa kitu kimoja bila kuwepo kigugumizi na chama chetu kimeshinda tunakwenda kufyeka pori mbele kwa mbele.”

Komu alisema hawakuwa na dhamira wala kusudio maalumu la kuzungumza maneno hayo na walianzia mbali lakini sauti iliyosikika ni sehemu tu ya mazungumzo yao.

Kuhusu madai ya kumdhuru Jacob

“Kilichosababisha tukaonekana tuna mpango wa kumdhuru (Jacob) ni kwa sababu hii sauti ilitoka kwa bahati mbaya na kila mtu akatafsiri kwa maana yake kwa sababu sisi tulisema kumtoa kwa hiyo tafsiri ya kudhuru imetolewa na watu,” alisema Komu.

Jacob awasamehe

Akizungumza na Mwananchi, Jacob alisema, “Kama chama kimesamehe na mimi ni sehemu ya chama, sina tatizo.”

“Wote wamekiri ila kama wangekataa ndiyo tungeweza kuomba msaada wa vyombo vya Serikali kama TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania).”

Jacob, ambaye pia ni diwani wa Ubungo alisisitiza, “Mimi sina tatizo lakini kama Serikali na vyombo vya dola vitaona kuna haja ya kuendelea mimi siwezi kuwazuia ni wao tu, maana kwangu adhabu iliyotolewa na chama nimeridhika nayo.”

Mwananchi liliwatafuta viongozi wa Jeshi la Polisi jana bila mafanikio.

Mnyika, Mwalimu wafafanua

Akifafanua zaidi, Mnyika alisema, “Kamati Kuu iliitishwa na ikafanya kikao chake juu ya tuhuma za utovu wa nidhamu wa wabunge hao na kuwakuta na hatia.”

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alipoulizwa sababu za kutowavua uanachama wabunge hao, alisema shabaha ya Chadema si kufukuzana na wanataka kila Mtanzania awe sehemu ya chama hicho. “Kamati Kuu iliwahoji na kuwatia hatiani na wakapewa adhabu. Kwa mujibu wa katiba yetu adhabu zipo nyingi si kufukuzwa tu. Hatupangiwi wakati gani kama chama tuchukue adhabu gani,” alisema Mwalimu.

Wakanusha matukio ya utekaji

Mnyika alisema chama hicho hakina mikakati ya utekaji au utesaji au mikakati mingine haramu na kueleza yanayozungumzwa dhidi yao ni propaganda zinazopaswa kupuuzwa.

“Kama ingekuwa kweli, nguvu yote ya dola ingeelekezwa kwetu. Hivi kwa nini Serikali haitaki wachunguzi binafsi kuchunguza matukio ya utekaji na upigwaji risasi,” alisema akitolea mfano tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’.

Tuhuma dhidi ya Mbowe

Mnyika pia alizungumzia Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema kuandamwa na baadhi ya wanachama kuwa hafai kukiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

“Mbowe ndiye kiongozi mkuu wetu na inafahamika kuwa ukubwa ni jalala, hivyo mambo kama haya kutupiwa ni kawaida. Hata mwenyekiti wa CCM pia anakutana nayo ila sisi kama Chadema tunafanya kila linalowezekana kumlinda mwenyekiti wetu,” alisema Mnyika.

Mwalimu naye aligusia hilo na kusisitiza wasipangiwe nani awaongoze kwa kuwa wanachama wanamtaka Mbowe.

Mipango ya Chadema

Mnyika alieleza kuwa katika kipindi hiki ambacho chama hicho hakitashiriki kwenye chaguzi ndogo, wataelekeza nguvu kwenye ujenzi wa chama kwa kufanya mikutano ya ndani na lengo likiwa kuiondoa CCM madaraka

Chanzo: swahilihub.com

No comments:

Post a Comment

Maoni yako