
Katika utaratibu wa sasa mabilioni ya Rais Kikwete hupitia katika benki za NMB na CRDB kwa ajili ya kuwakopesha wananchi kupitia vikundi vyao zikiwemo Vyama vya Kuweka na Kukopa (Saccos).
Akifungua maonyesho ya Vicoba yaliyoandaliwa na Taasisi ya Umoja Aids Control and Community Youth Development (Uyacode), Lowassa alisema fedha hizo zikipitia Vicoba utakuwa ukombozi mkubwa kwa wananchi maskini.
Lowassa wamewataka wana–Vicoba kuwashawishi wabunge wao ili walishawishi Bunge ili fedha hizo ziweze kupitia vicoba vinginevyo wawanyime kura.
“Mbunge ambaye atashindwa kushawishi Bungeni ili mabilioni ya JK yaweze kwenda moja kwa moja kwa vicoba msimpe kura,” alisema Lowassa.
Alisema wabunge watakaoshindwa kufanya hivyo wasipewe kura kwa sababu watakuwa wameshindwa kuwasaidia wananchi wao katika kupambana na umaskini.
Bila kueleza ubaya wa mfumo huo wa sasa wa utoaji wa mabilioni ya JK, Lowassa alisema yeye ni muumini wa Vicoba anayeamini kwamba unasaidia wananchi wa kawaida katika kupambana na tatizo la ajira.
“Vicoba ni ukombozi wa umaskini, nami sasa nimekuwa muumini wa Vicoba kwani mfumo huu utawasaidia kwa kiasi Watanzania katika vita dhidi ya umaskini,” alisema Lowassa.
Lowassa aliendelea kutetea msimamo wake kwamba ajira ni bomu ambalo linaweza kuripuka wakati wowote kutokana na vijana wengi kukosa ajira.
“Baadhi ya watu naona hawakunielewa vizuru, wakazungumza sana, lakini ni lazima tufahamu kwamba tatizo la ajira bado ni kubwa na tunatakiwa kujadiliana namna tunavyoweza kupambana nalo,” alisema Lowassa.
Alisema kukaa kimya kama vile hakuna tatizo linaliwakabili Wanzania walio wengi itakuwa vigumu kuliondoa.
Alisema kuwa kama nchi zilizoendelea kama Marekani kuna mjadala mkubwa wa tatizo la ajira, iweje nchi maskini kama Tanzania ishindwe kujadili tatizo hilo.
“Marekani ni nchi tajiri lakini wanazungumza kuhusu tatizo la ajira katika nchi yao sisi akina nani hadi tushindwe kulizungumzia,” alisema Lowassa.
Aliwaahidi wanachama hao kwamba atawashawishi watu wengine kuunga mkono mpango wa Vicoba kwani unaonyesha kuwa na manufaa katika kupambana na umaskini.
Akimkaribisha Lowassa, Ofisa Miradi wa Uyacode, Margareth Mapunda alisema maonyesho hayo yanashirikisha vikundi vya Vicoba 100.
Alisema lengo la maonyesho hayo ni kutangaza shughuli mbalimbali zinazofanywa na vicoba ili kupata masoko.
Alisema maonyesho yatakayochukua siku saba yanawashirikisha wana-vicoba wa mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani.
“Pia tunaadhimisha miaka 10 tangu taasisi ya Uyacode ilipoanzishwa mpango wa Vicoba,” alisema Mapunda.
Alisema tangu kuanzisha kwa vicoba wananchi wamehamasika kuweka akiba katika vikundi vyao ikiwa ni njia ya kukabiliana na umaskini.
Na Raymond Kaminyoge. Mwanachi



No comments:
Post a Comment