Ruto anataka asilimia 50 ya nyadhifa hizo na amemwambia Kenyatta kwamba atagawa nyadhifa zilizosalia na vyama vingine katika muungano huo kama vile New Ford Kenya ya Eugene Wamalwa na Narc ya Charity Ngilu.

MGOMBEA Urais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amekuwa katika ziara zisizokoma za nchi za Afrika Mashariki kwa lengo la kutafuta uungwaji mkono wa marais wa nchi hizo.
Tayari amekutana na kufanya mashauriano na viongozi wa Tanzania, Burundi, Sudan Kusini miongoni mwa wengine, na bado anaendelea na ziara hizo.
Huku nyumbani, baadhi ya viongozi na wagombea wa urais kama vile Naibu Waziri Mkuu, Musalia Mudavadi na Martha Karua wanatoa onyo kali na ushauri kwa Wakenya wasidhubutu kuwachagua washukiwa hao wasije wakajuta.
Mudavadi anasema kwamba Wakenya wakifanya makosa ya kuwapa Kenyatta na William Ruto jukumu la kuwaongoza, nchi itakuwa katika mashaka makubwa katika nyanja za kiuchumi na kisiasa ulimwenguni. Kiongozi huyu hapo awali alikuwa akiunga mkono wawili hao na hata kuwaambia Wakenya kuwa mzigo wanaobeba viongozi hao katika Mahakama Kuu ya Kimataifa ya ICC huko The Hague, Uholanzi, ni mzigo wa Wakenya wote.
Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka kwa kuwa bado anatarajia kwamba kuna uwezekano wa kuwa katika muungano na washukiwa hao, haswa Ruto, hataki kamwe kugusia suala hili. Juzi, katika mkutano wa kisiasa, aliukejeli muungano ambao sasa unayumbayumba kati ya Kenyatta na Ruto. Mazungumzo ya muungano kati ya viongozi hao wawili yamepigwa na dhoruba kali kwa sababu hawajakubaliana kuhusu nyadhifa za mawaziri na maspika wa Bunge na Seneti.
Ruto anataka asilimia 50 ya nyadhifa hizo na amemwambia Kenyatta kwamba atagawa nyadhifa zilizosalia na vyama vingine katika muungano huo kama vile New Ford Kenya ya Eugene Wamalwa na Narc ya Charity Ngilu.
Kenyatta hataki kusikia hayo na anasema anataka nyadhifa zote zigawanywe miongoni mwa vyama vyote. Wakenya wanatazama jinsi mzozo huu utatatuliwa.
Musyoka alimpa Ruto ushauri wa bure kwamba, asipoteze muda wake kwa kujiunga na Kenyatta kwa sababu hawezi kutimiziwa aliyoahidiwa.
Musyoka yuko katika njia panda na anataka kufanya kila awezalo kupata mgombea mwenza, juhudi ambayo haimpi lepe la usingizi kipindi hiki.
Mudavadi naye ameona mwangaza kama Paulo wa Bibilia na sasa ana mahubiri mapya baada ya kutembelea Damascus ya siasa.
Alipotafakari zaidi kuhusu utawala wa Kenyatta na Ruto, Mudavadi aligundua kwamba, hakuna uzuri wowote utakaotokana na kuchaguliwa kwao. Ili adhihirishe msimamo wake mpya kwa Wakenya wanaopinga uongozi wa wanasiasa hao wanaosubiri kufikishwa katika Mahakama Kuu ya Uhalifu wa Kimataifa, The Hague kuanzia Aprili 10 mwaka ujao, mwanasiasa huyu anasema kinagaubaga kwamba hamna haja kuwachagua Kenyatta na Ruto.
Anashangaa kwamba baadhi ya wanasiasa wanaounga mkono washukiwa hao, wanakosa kuona jinsi ambavyo uhusiano wa Kenya na mataifa mengine utakavyoathiriwa vibaya na utawala wa wawili hao ikiwa watachaguliwa. Anachelea Kenya kutengwa na mataifa mengine na kupelekea uchumi kudorora kwa kuwa kutengwa kule kunaweza pia kuambatana na kuwekewa vikwazo vya kiuchumi.
Karua, bila kusita anasema Kenyatta na Ruto kamwe wasichaguliwe kwa kuwa ni washukiwa wanaosubiri kufikishwa kortini kujibu mashtaka ya mauaji, ubakaji na kupanga ghasia zilizozua mapigano baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.



No comments:
Post a Comment