Na Rajab Ramah, Nairobi
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi Nancy Omala anakumbuka kwa uchungu wakati wezi walipompora kompyuta yake ya mkononi wakati akitoka duka la kahawa katika Wilaya ya Kati ya Biashara jijini Nairobi.

Wakaazi wa kitongoji cha Eastleigh mjini Nairobi wakitembea katika wilaya ya biashara. Karibuni Nairobi itakuwa na kamera za ulinzi ili kuzuwia uhalifu na kusaidia katika uchunguzi wa polisi. [Na Simon Maina/AFP]
Omala, mwenye umri wa miaka 25, alikuwa ndio kwanza amemaliza kufanya masawazisho ya mwisho ya kazi yake ya shule na alikuwa karibu aiwasilishe ili aweze kuhitimu.
"Kwa bahati mbaya, sikuwa na kopi ya akiba ya kazi hiyo", aliiambia Sabahi. "Wezi walinipora maisha yangu na ilikuwa pigo kwa kazi yangu." Alisema kuwa wezi wamemfanya asiweze kuhitimu mwezi wa Agosti iliyopita, kwa hivyo ilibidi aanze tena kazi yake ili aweze kuhitimu mwakani.
"Nyuso zao bado zimo katika akili yangu," alisema. "Nilielezea wasifu kwa polisi, lakini ni vigumu kuweza kuwapata. Hata kama polisi wangewapata, bado ni vigumu kuthibitisha kuwa walikuwa wao kwa sababu hakukuwa na shahidi wengine."
Maafisa wanatumai kuwa hadithi kama ya Omala zitapungua sana kutokana na kuwekwa kwa kamera za ulinzi 41 katika maeneo yenye uhalifu mwingi jijini.
"Tulizitambua sehemu za mwanzo kuwekwa kwa kamera kuwa maeneo ya uhalifu," Waziri wa Mji Mkuu Nairobi Jamleck Kamau aliiambia Sabahi. "Polisi, wafanya biashara jijini na wananchi walitusaidia kutengeneza ramani ya maeneo haya."
Mradi huu umetoa kipaumbele kwa maeneo yenye msongamano mkubwa jijini, Kamau alisema, na maeneo yatakayofungwa kamera hizo ni pamoja na Kituo cha Mabasi Nchini cha Machakos, Soko la Muthurwa, Soko la Gikomba, Hospitali ya Taifa ya Kenyatta, Barabara ya Kirinyaga katikati ya mji wa Nairobi na eneo lote la Wilaya ya Kati ya Biashara.
Alisema kuwa kuweka "mfumo wa ulinzi mjini" karibu na majengo, mitaa na makutano makubwa kutasaidia kuzuwia uhalifu na makosa ya usalama barabarani. Mradi huo utagharimu shilingi bilioni 8.5 (dola milioni 99) na unatarajiwa kumalizika ndani ya miezi mitatu, na awamu ya kwanza itaanza kufanyakazi mwezi wa Januari.
Kupambana na ugaidi, uhalifu na wakosaji wa usalama barabarani
Mfumo wa Kamera zilizounganishwa na televisheni (CCTV) utakuwa ukionesha video moja kwa moja ambazo zitakuwa zinarekodiwa na kuhifadhiwa ili kuangaliwa upya baadaye. Kamau alisema kuwa kamera hizo zitazuwia tabia mbaya za kijamii na kuweza kusoma nambari za gari na data nyengine za utambulisho wakati wa kutendeka kwa makosa.
Zaidi ya hayo, Kamau alisema kuwa kamera za CCTV zitasaidia kupambana na ugaidi. "Magaidi mara kwa mara wamekuwa wakiilenga Nairobi," alisema. "Tunatumai kuwa vifaa hivi vitawatimua, lakini wale watakaothubutu kujaribu matendo yao ya kiwoga hapa watakamatwa."
Mkuu wa polisi mjini Nairobi Moses Ombati alikubali kuwa kamera hizo zitakuwa nyenzo ya thamani kwa maafisa jijni. "Tuna imani kuwa mfumo huu utaisaidia polisi kugundua na kuzuwia uhalifu [na] hii itamaanisha kupungua sana kwa uhalifu mkubwa jijini na maeneo jirani," aliiambia Sabahi.
"Pale ambapo tayari uhalifu utakuwa umeshatendeka, itakuwa rahisi kuchunguza na kuwakamata watendaji makosa hayo kwa kutumia mambo yatakayonaswa na CCTV," Ombati alisema.
Kamanda wa usalama barabarani Benson Kibue alisema kuwa vifaa hivi vitasaidia kupunguza msongamano wa magari na kuwakamata watendaji wa makosa ya usalama barabarani. "Kukiwa na CCTV kila mahali, tutasimamia mtiririko wa vyombo katika barabara zetu ili kudhibiti usalama barabarani kwa jumla jijini, jambo ambalo litatusaidia kuondosha msongamano," alisema.
Mwenyekiti wa Wilaya ya Kati ya Biashara Nairobi Timothy Muriuki alisema kuwa kamera zitasaidia biashara mjini Nairobi na kusaidia kuufanya mji uwe wa ushindani.
"Wahalifu wameanza kulenga biashara, na kuufanya mji wa Nairobi kuwa adui kwa wanachama wetu," aliiambia Sabahi. "Kuna wale waliolazimika kuacha biashara na wale waliomudu kuanzisha mifumo yao wenyewe ya uchunguzi, lakini hii ni gharama sana [kwa muda mrefu]. Huu ni mpango uliokuja kwa wakati ambao utakuwa ni msukumo mkubwa kwa Nairobi."
Baadhi ya wananchi wanasema jicho linalotizama la serikali linaweza kugharimu biashara katika pesa za jiji.
"Wengi wa wateja wetu ni watu wa faragha sana na wanachukia wazo la kuwa wanaangaliwa au kusimamiwa," alisema Mathews Njoroge, dereva wa taksi katikati ya jiji. "Kamera hizi zitatuibia faragha yetu na yao. Hii ina maana kuwa [wateja] watahama mji ili kuepuka macho ya wanaowafuatilia kwa karibu sana na kwa hivyo biashara kukosa wateja."
Waziri wa Mji Mkuu Nairobi, Jamleck Kamau alitoa wito kwa wananchi wasiguswe kupita kiasi juu ya mfumo wa CCTV na alisema kuwa faida zake ni kubwa kuliko hasara. "Hakuna sababu kwa nini watu wawe na wasiwasi kuhusu uvumbuzi huu, isipokuwa wale tu watakaokuwa wametoka kwa ajili ya ufisadi," alisema.
Chanzo http://sabahionline.com/



No comments:
Post a Comment