
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Bandari hizo zinajengwa katika mikoa ya Rukwa, Kigoma na Katavi. Pinda anataka TPA imfukuze kazi mkandarasi huyo baada ya kushindwa kuikamilisha kwa zaidi ya miaka miwili.
Mkandarasi huyo, Kampuni ya Modspan Enter Limited ya Dar es Salaam ilishinda zabuni ya kujenga bandari ndogo za Kipili wilayani Nkasi (Rukwa) na Karema (Katavi) na bandari za Lagosa na Sibwesa mkoani Kigoma zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Waziri Mkuu alisema mkandarasi huyo amekosa uwezo wa kuimudu kazi hiyo. Alitoa agizo hilo mjini Mpanda baada ya kuarifiwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk Rajab Rutengwe kuwa mkoa huo hauna bandari ya kisasa katika mwambao wa Ziwa Tanganyika kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria na mizigo.
Waziri Mkuu alifahamishwa pia kuwa pamoja na Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kuanza kujenga bandari kijijini Karema, lakini kwa sasa ujenzi umesimama baada ya mkandarasi kushindwa kuimudu kazi kwa kukosa uwezo.
Kama bandari hiyo ingekamilika, ingefungua soko kubwa la bidhaa mbalimbali katika nchi jirani na kuvutia wawekezaji katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika wenye mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi.
Kutokana na maelekezo hayo, Pinda alishangazwa na kuhoji iweje mkandarasi mwenye uwezo huo mdogo ambaye ameshindwa kuimudu kazi hiyo ashinde zabuni za kujenga bandari tatu za Kipili, Karema na Sibwesa katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika.
“Hatuwezi kumvumilia na tayari nimeshaagiza (TPA) kumwachisha kazi mara moja mkandarasi huyu ili atafutwe mwingine kwa kufuata kanuni za kutangaza zabuni, lakini kinachonishangaza hapa ni vipi mkandarasi huyu aliweza kushinda zabuni wakati hana uwezo?” Alihoji.
Wakati akihoji hivyo, Dk Rutengwe alimfahamisha kuwa hivi karibuni mkandarasi huyo ‘alibambwa' na vyombo vya dola, akijiandaa kutorosha vyombo vyake vya ujenzi kusikojulikana, lakini mkandarasi huyo tayari amelipwa fedha zote za ujenzi wa miradi hiyo.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alitembelea na kukagua miradi hiyo ya ujenzi wa bandari hizo ndogo, ambapo alieleza wazi kuwa kutofurahishwa kwake na mwenendo wa ujenzi wa bandari hizo mbili za Kipili na Karema na zile za Sibwesa na Lagosa zilizopo mkoani Kigoma, kwani hata fedha za ujenzi wa miradi hiyo ilikuwa imeshatengwa.
Hata hivyo, katika ziara hiyo ya Naibu Waziri ya kutembelea ujenzi wa miradi ya ujenzi wa bandari hizo, katika hali isiyokuwa ya kawaida Mhandisi Msimamizi wa TPA na Mhandisi wa miradi hiyo ya ujenzi, walishindwa kujizuia na kujikuta wakilumbana kwa kurushiana shutuma nzito mbalimbali mbele ya Dk Tizeba, kuhusu kudorora kwa ujenzi wa miradi ya ujenzi ya bandari ya Kipili na Karema.
Ilibainika kuwa mkandarasi huyo ndiye aliyeshinda pia zabuni ya ujenzi wa bandari ya Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa, ambapo sasa imelazimika kubomolewa baada ya kujengwa chini ya kiwango.
Mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya alifanya ziara ya kukagua ujenzi wa bandari ndogo za Kipili na Karema na kutoridhika na kusuasua kwa ujenzi wa miradi hiyo.
Chanzo: Gazeti la HabariLeo



No comments:
Post a Comment