Na Hassan Muse Hussein, Garowe
Hassan Mohamed Jama, mwenye umri wa miaka 53, amekuwa akiendesha maisha kama anayeghishi huko Bosaso na Garowe kwa miaka 20 iliyopita.

Maofisa kutoka Serikali ya Mpito ya Shirikisho wakionyesha nakala ya pasipoti ya kibiometriki mwezi Novemba 2006. Hali ya kiwango cha juu kabisa kilichofikiwa katika sayansi ya teknolojia ya pasipoti inachukua nafasi ya nyaraka za zamani ambazo zilikuwa rahisi kughushi. [Tony Karumba/AFP]
yeye hutengezeneza pasipoti za kijani za zamani zilizotumika chini ya utawala uliopita, pasipoti nyekundu za kidiplomasia, diploma za chuo kikuu, vyeti vya kuzaliwa na hati miliki. Jama, ambaye bado anafanya kazi katika biashara hii, alisema kwamba pasipo nyaraka za kughushi maisha yangekuwa magumu kwa Wasomali wengi.
"Wakati tulipoanza kazi hii, nchi haikuwa na mahali pa watu kwenda kupata nyaraka hizi na Wasomali walikuwa wakisafiri kila siku kwa sababu walikuwa wakipata ufadhili wa masomo," Jama aliiambia Sabahi. "Tulikuwa tukifanya kazi kama serikali za mitaa na Wizara ya Elimu, tulijaza mapengo yote hayo."
"Tunatengeneza pasipoti za zamani za kijani kwa hadi dola 100. Tunatoza dola 300 kutengeneza vyeti vya chuo kikuu kama kile cha Chuo Kikuu cha Taifa cha Somali, ingawa ni vigumu kununua viandikia halisi. Vyeti vya vyuo vikuu ambavyo vilitengenezwa baada ya kuanguka kwa nchi vinagharimu dola 60," alisema.
Ingawaje pasipoti za zamani na diploma za shule hazitambuliki tena rasmi kama halali na serikali ya shirikisho na utawala wa mkoa, watu bado wanategemea nyaraka za kughushi. Jama alisema yeye huwaona watu takribani 20 kila siku wanaotaka vyeti vya kughushi na pasipoti ya kijani ya zamani, ambayo inaweza kutumiwa kusafiria katika baadhi ya nchi ambazo hazitekelezi upigwaji marufuku.

Hassan Mohamed Jama akipiga muhuri pasipoti za Somalia zilizoghushiwa kwa kutumia vifaa vilivyoibiwa kutoka kwenye ofisi za serikali baada ya serikali kuu kuanguka mwaka 1991. [Hassan Muse Hussein/Sabahi]
"Watu wamezoea huduma zetu ambazo zinawawezesha kupata pasipoti, cheti cha chuo kikuu au cheti cha kidato cha sita ndani ya dakika 20," alisema. "Hilo ndilo wanaloona ni muhimu na tunategemea hilo ili kuwalea watoto wetu."
Alisema Wasomali wanaoghushi wana mihuri yote inayotumiwa na idara za serikali iliyopita, na kutumia saini zilizo nyingi za viongozi wa serikali iliyopita ambako kumeleta mchanganyiko katika nchi za kigeni.
"Tunalazimika kujifunza jinsi ya kughushi saini hizo ili kutoa nyaraka ambazo zinaonekana ni halali kwa sababu nchi nyingi duniani zinaweka saini za viongozi wa serikali katika jalada [ili kuthibitisha]," Jama alisema.
Hatua za kuzuia kughushi
Ingawa mfumo wa udanganyifu umeshamiri nchini Somalia kwa miongo miwili, kuna baadhi ya ishara kwamba serikali inachukua hatua za kupambana na tatizo hilo.
Kwanza, Serikali ya Mpito ya Shirikisho ya Somalia ilitengeneza pasipoti mpya za biometriki mwaka 2006 na kubadilisha rangi kuwa bluu. Serikali iliweka mtambo wa kuchapisha pasipoti huko Mogadishu mwaka 2010, kuhamisha kutoka Falme za Kiarabu , kuharakisha huduma ya upatikanaji wa pasipoti.
Mwaka 2011, serikali ilizuia rasmi matumizi ya pasipoti za zamani za rangi ya kijani kwa ajili ya safari za kimataifa au shughuli za kibiashara, hata hivyo, baadhi ya nchi hazitekelezi hilo.
"Waliokuwa wakifanya kosa la kughushi ni kikwazo kwa maendeleo ya nchi kwa kuanzisha sifa mbaya kwa pasipoti za nchi," alisema Ali Abdi, kiongozi katika tume ya shirikisho la pasipoti huko Galkayo. "Walipatikana wakitengeneza pasipoti kwa ajili ya watu wa kutoka nchi za nje katika masoko."
"Serikali ya shirikisho sasa imeziomba nchi nyengine duniani kote kuzikataa pasipoti za zamani za Somalia na kuzikubali mpya," aliiambia Sabahi. "Badiliko hili linaonekana kwa sababu kila siku tunasajili kiasi cha watu 100 wanaotafuta pasipoti mpya."
Mwaka 2010, Wizara ya Elimu ya jimbo ya Puntland pia ilianzisha programu ya kuzuia kughushiwa kwa vyeti vyake vya chuo kikuu, mkurugenzi wa mafunzo wa wizara Ali Farah aliiambia Sabahi.
Alisema kuwa wizara imeikodi kampuni ya Malaysia kutengeneza diploma zilizochapishwa kwa kutumia karatasi maalumu zenye alama za usalama katikati ambazo haziwezi kughusiwa. Diploma zilitumwa kwa vyuo vikuu vyote vya ndani na kwa nchi za eneo hilo ambapo wanafunzi wa Somalia huwa wanatafuta ufadhili wa masomo kwa kuendela na elimu yao, alisema.
"Tuliamua kufanya vile kwa sababu tuliziona diploma zetu zikitengenezwa kienyeji na hata kughushiwa huko Sudan," Farah alisema. "Tuliamua kupambana na tatizo hilo na tulikataa kutangaza kampuni iliyotengeza [diloma mpya] ili kuzuia asiwe na mawasiliano nao jambo ambalo linaweza kuzidisha kughushi."
"Mwaka 2012 tuligundua kjuwa matukio ya kughushi yamepungua kwa mujibu wa vyuo vikuu vya ndani vilivyofanya kazi pamoja nasi ili kupambana na tatizo hilo," alisema.
Mahitaji ya kughushi lazima yatokomezwe
"Wakati wa kipindi cha machafuko, [watu wanaoghushi] walitoa huduma ambazo serikali inatoa kwa watu wake. Watu wangeweza kupotea kama huduma zilikuwa hazipatikani," alisema Abdi Abdullahi Sheikh, mkazi wa Garowe mwenye umri wa miaka 24 - ambaye anakwenda shule ya Upili ya Gamboi.
"Kwa mfano, pasipoti zilkuwa zinapatikana kirahisi bila ya matatizo mengi au kuchelewa kwa safari," aliiambia sabahi. "Zilirahisisha idadi ya Wasomalia ambao walitembea duniani kote kwa biashara na elimu katika miaka 20 iliyopita."
Ni vigumu kwa serikali kupambana kikamilifu na biashara ya kughushi ambayo imekuwa ikiendelea kwa zaidi ya miaka 20 sasa, alisema mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Garowe, Saleban Jama. Serikali inaweza kubadilisha utamaduni na kuwafanya Wasomali wafahamu kuwa wakati umefika kuachana na kughushi, alisema, lakini inapaswa kuwa na mbadala wake.
"Kwa mfano, vyeti vya kuzaliwa, vibali vya ndoa, leseni za udereva na vitu vyote hivyo havitolewi na serikali kuu ya Mogadishu kwa sasa," Jama aliiambia Sabahi. "Kwa hivyo, mtu yeyote anayezitaka au anahitajika awe nazo ili aweze kusafiri nje anazipata kutoka kwao [wanaoghushi]. Serikali inapaswa kuziba jukumu hilo kwa sababu kughushi kulinawiri kutokana na mahitaji [ya huduma] kwa hivyo ikiwa zinatolewa, watu hawatataka kughushi."
Via sabahionline.com



No comments:
Post a Comment