Mhojiano yalifanywa na Deodatus Balile, Dar es Salaam
Edward Hoseah, mpambanaji wa juu kabisa wa Tanzania dhidi ya rushwa katika viwango vyote vya serikali, anasema nchi inaweza kujinasua na athari za ubovu wa rushwa na kuwa moja ya nchi zenye rushwa ndogo kabisa duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Edward Hoseah akizungumza na mashirika ya asasi za kijamii juu ya mafanikio ya taasisi hiyo hadi sasa katika Hoteli ya Mövenpick jijini Dar es Salaam mwezi Machi 2012. [Na Deodatus Balile/Sabahi]
Hoseah anaongoza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini na pia ni mwenyekiti wa Bodi ya Umoja wa Afirika (AU) ya Kupambana na Rushwa.
Tangu alipochukua nafasi ya mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU mwaka 2006, taasisi hiyo imesaidia sana kupunguza rushwa na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika orodha ya rushwa duniani kote, Hosea anaiambia Sabahi katika mahojiano.
Lakini licha ya mafanikio hayo, Hosea anasema kuwa taasisi yake inahitaji na kupewa mamlaka zaidi ili kuwa ya mafanikio zaidi, ikiwa ni pamoja na nguvu za kushitaki.
Sabahi: Ziko wapi kazi kuu zilizokabidhiwa TAKUKURU?
Edward Hoseah: Wajibu wetu mkuu ni kuzuia rushwa nchini. Tunaishughulikia rushwa kutoka pande tatu. Kwanza ni kuzuia, ambako kunajumuisha usimamiaji wa kiwango [kikubwa] cha uhawilishaji fedha na kuchunguza mienendo ya kisasa [juu ya vipi watu wanabadilishana fedha].
Upande wetu wa pili ni elimu kwa umma. Tunanyanyua mwamko wa watu kuhusu maovu ya rushwa, na tunahamasisha majadiliano na mijadala juu ya rushwa ambayo huwapa watu uwezo wa kujua haki zao.
Uwanja wetu wa tatu ni kuzuia makosa yasitendeke. Katika uwanja huu, tunachunguza na kuwashitaki wale wanaojihusisha na vitendo haramu.
Sabahi: Utaratibu gani mnao wa kuchunguza rushwa?
Hoseah: Tunao Mkakati wetu wa Taifa wa Kupambana na Rushwa, ambao unafanyakazi vizuri. Ninaishukuru serikali kwa sababu, katika muda wa miaka 10 au zaidi, imeiwezesha TAKUKURU kufungua ofisi zake katika kila wilaya. Nchi hii inazo wilaya 133, na tunao maafisa katika kila moja. Ofisi zetu zinafuatilia kwa karibu vidokezo vinavyopewa na wanaotoa taarifa.
Sabahi: TAKUKURU ipo tangu mwaka 1974. Mmefanikia vipi katika nafasi yako kuwa mkurugenzi mkuu?
Hoseah: Kunaweza kuwepo na kukosolewa [kuhusu utendaji wetu], lakini kiwango cha rushwa Tanzania kinashuka kila siku. Rushwa ilikuwa kileleni mwake mwaka 2009, lakini nitaitaja miaka hiyo mitatu iliyopita ili kuonyesha mwenendo uliochapishwa na mashirika ya kimataifa ambayo yanatambua juhudi zetu.
Orodha ya Ibrahim ya Utawala Afrika iliiweka Tanzania katika nafasi ya 15 ya rushwa ndogo kati ya idadi ya nchi 53 za Afrika katika ripoti yake ya mwaka 2010. Katika ripoti ya mwaka 2011, tuliimarika hadi nafasi ya 13 na katika kipindi cha mwisho kabisa, tumekuwa wa 10. Sitaki kuzitaja nchi jirani zetu za Afrika Mashariki, lakini inatosha kusema kwamba sisi tunaongoza, na ninachojua ni kwamba nchi inayofuatia kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki iko katika nafasi ya 19.
Unapoangalia katika Ripoti ya Uwazi wa Kimataifa kwa Mtazamo wa Rushwa, maendeleo yetu ni ya kusifiwa. Tulikuwa katika nafasi ya 116 mwaka 2010, tukaimarika kufikia wa 110 mwaka 2011 na nafasi ya 102 , mwaka 2012. Kwa jumla, mwendendo wetu unatia moyo kwa vile tunapunguza kiwango cha rushwa kila siku.
Hii haitokezei kwa miujiza. Sisi ni nchi ya kwanza barani Afrika kuwashitaki mawaziri wawili mwaka 2009 na nafasi kuu za serikali kama vile makatibu wakuu. Shinikizo la vyombo vya habari lilipelekea kujiuzulu kwa waziri mkuu, Edward Lowassa, [ambaye] alihusika katika kashfa ya rushwa mwaka 2008. Kulikuwa na mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri mwaka 2012 ambayo yalipelekea kufukuzwa kwa mawaziri wanane. Wafanyabiashara wakuu wa kike na wa kiume wako mahakamani kwa kuhusisha na kashfa za ufisadi, kama tunavyozungumza hivi sasa.
Kwa hakika tumefanya mengi, ingawaje mengi zaidi yanahitajika kufanyika. Kila Mtanzania sasa yuko macho linapokuja suala la rushwa. Wanaangalia jicho kila kipembe.
Sabahi: Bado, umma hauonyeshi kuridhika na kazi inayofanywa na TAKUKURU. Jawabu lako ni nini?
Hoseah: Kwa chombo chochote cha kupambana na rushwa ili kiwe na ufanisi na kujitosheleza, kuna kanuni au hali kadhaa ambazo lazima ziwepo. [Hitaji] Mojawapo wa [taratibu za] msingi kwa chombo kama hicho kufanya kazi vizuri na kuchukuliwa na wananchi kama chombo chenye uwezo, ni uhuru wake katika kushughulikia rushwa kubwa.
Hiyo haimaanishi kwamba rushwa ndogondogo hazina umuhimu -- sio hata kidogo. Kinyume chake, rushwa za kiwango kidogo zinawaathiri watu wengi zaidi, lakini ikiwa hatua za kuzuia makosa yasitendeke [kama vile muda wa kukaa jela] haziimarishwi ipasavyo na kwa wakati katika kesi za rushwa [zinazohusu viwango vikubwa vya fedha], kazi zote za kuzuia zinakuwa hazina maana.
Sabahi: Unakusudia kusema kwamba TAKUKURU haina mamlaka au si huru?
Hoseah: Nazungumzia uwezo wa kutumia madaraka au wajibu wetu bila ya kuingiliwa kati au kuhamasishwa na wengine nje ya taasisi, ambalo ni jambo la lazima kabisa.
Kupambana na ufisadi ni kupambana na watu wenye nguvu kubwa, wenye pesa nyingi na ambao, katika hali nyingi, ndio wanaohusika na kesi kubwa za ufisadi. Kwa hiivyo, [kuwa na ufanisi] tunahitajia kuusimamia mchakato wa kuwashitaki mafisadi, jambo ambalo sivyo lilivyo kwa mujibu wa sheria za sasa.
Ninachosema ni kwamba tunakosa uwezo wa kushitaki. Hili [linatuzorotesha] katika kupambana na rushwa kwenye nchi hii.
Sabahi: Kwani nani mwenye jukumu la kufungua kesi za ufisadi?
Hoseah: Kisheria, mamlaka ya kufungua kesi kwenye nchi hii yako kwenye mikono ya Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali (DPP).
Tunapeleleza kesi nyingi sana, tunakuja na ushahidi wa wazi kabisa wenye dalili zote kwamba kesi hizo zinaweza kushinda zikipelekwa mahakamani, lakini tunapaswa kuuwasilisha ushahidi wetu kwa DPP (ambako wanaamua kesi gani ifunguliwe). Katika mchakato huo, baadhi ya kesi zinatupwa na nyingine zinazimwa. Kimsingi, tukishakamilisha upelelezi, jambo huwa liko nje ya mikono ya TAKUKURU.
Sabahi: Mbali na nguvu za kufungua mashitaka, kipi kingine ambacho kingeliweza kuifanya taasisi yako kuwa na ufanisi zaidi?
Hoseah: Tunastahiki kuwa na nguvu, nguvu ya wazi kabisa kwa ajili ya kuzuia, elimu, upelelezi na uendeshaji wa kesi [za ufisadi].
TAKUKURU haiwezi kufanya kazi ikiwa imejitenga. Kwa hivyo, tunahitaji pia ushirikiano na dola na wahusika wengine kwenye uwanja huu, ndani na nje ya nchi. TAKUKURU imeanzishwa kwa sheria iliyopitishwa na bunge, kwa hivyo udumishwaji wake haujalindwa. Inahitaji kuanzishwa kwa sheria za nchi, katiba, kwa ajili ya udumishwaji.
Usalama wa uhakika kwa maafisa wa TAKUKURU na utaratibu wa uteuzi wa katiba [unapaswa] uwe wa lazima. Kwa sasa, kwa ajira yoyote inabidi tuwasilishe maombi kwa hazina kuu. Hili linapunguza uaminifu na uendeshaji wa taasisi hii muhimu kabisa.
Mkuu wa TAKUKURU na wafanyakazi wake lazima wake na kinga dhidi ya kufunguliwa mashitaka ya hukukia na kihalifu kwa [hatua wanazochukua] kwenye [eneo la] mamlaka yao. TAKUKURU lazima ipate fedha zake moja kwa moja kutoka mfuko wake uliotengewa maalum (kuliko) kutengewa kupitia ofisi ya rais (chini ya Idara ya Utawala Bora).
Sabahi: Nini kimefanyika kuyatatua mapungufu haya?
Hoseah: Nimeshayaeleza yote haya kwa serikali, kwa bunge na katika matukio kadhaa za umma. Wote wananipa ahadi ya kuimarisha. Nina hakika kama nikisikilizwa, TAKUKURU inaweza kuubadilisha ufisadi kwenye nchi hii kwa kipindi kifupi tu.
Tunaweza kuwa nchi yenye kiwango kidogo cha ufisadi duniani, ikiwa tutapewa nguvu za kushitaki. Kwa muda wote hili ndilo tunalolilia, na tukipewa tu, tunaweza kuutokomeza ufisadi nchini.
Chanzo: sabahionline.com



No comments:
Post a Comment