Na Adnan Hussein, Mogadishu
Serikali ya Somalia inapanga kupeleka kikosi imara cha askari polisi 1,300 mwishoni mwa mwezi wa Mei ili kusaka wanachama wa al-Shabaab Mogadishu yote wakiwa na lengo la kuzuia mashambulizi na mauaji dhidi ya wanaharakati wa amani, vikosi vya usalama na maafisa wa serikali.

Askari wa Kikosi cha Polisi cha Somalia wakitoa saluti tarehe 18 Januari kabla ya kuingia ndani ya ndege kuelekea Djibouti kushiriki katika kozi ya mafunzo ya miezi mitatu. [Na Stuart Price/AU-UN IST/AFP]
"Miongoni ya kazi za kikosi chetu kipya ni kuweka sheria ya kutotoka nje, kuendesha misako, kuzuia mashambulizi, kulinda viongozi wa umma na kulinda [vituo vya polisi katika vitongoji]," Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa wa Somalia Abdikarim Hussein Guled aliiambia Sabahi.
"Askari wake watakuwa tofauti na vikosi vyengine kwa sababu ya sare zao za kipekee, vifaa na magari, pamoja na sababu ya kuwa wao watakuwa wakipokea mafunzo yanayoenelea ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha viwango vyao vya ukakamavu."
Kitengo cha polisi maalumu tayari kilishapatsa mafunzo nchini Somalia na nje katika matayarisho ya kuaanza kazi kwao, Guled alisema. Watapelekwa katika magari 120 yaliyopakwa rangi inayozitofautisha na wakiwa na zana zenye redio za kisasa na zana za kutoa tahadhari.
Kitengo hiki ni sehemu ya kampeni ya serikali ya shirikisho ili kuimarisha usalama na operesheni za kupambana na ugaidi mjini Mogadishu.
Kitengo cha polisi kitafanya kazi sambamba na operesheni zilizoratibiwa na kitengo imara maalumu cha kupambana na ugaidi cha askari 1,000 kilichoundwa na Wizara ya Ulinzi na kutolewa kutoka matawi kadhaa ya vikosi vya silaha na shughuli za usalama. Kitengo cha jeshi cha kupambana na ugaidi kilipangiwa kupelekwa Mogadishu mwishoni mwa mwezi wa April, lakini kikaahirishwa hadi katikati ya mwezi wa Mei.
Kikosi cha polisi kitakuwa na silaha na kitafanya doria za usalama mchana na usiku, alisema Mukhtar Hassan Mohamed, mkuu wa idara ya usajili na usimamizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa.
"Watashiriki katika operesheni za kudumisha amani, kusafisha mabaki ya kikundi chenye msimamo mkali na hasa kuziba maeneo ambako vikundi vya mauaji vinasadikiwa kujificha," aliiambia Sabahi. "Miongoni mwa kazi zao za kitaifa ni kuwalenga wauaji wanaokimbia maeneo ya uhalifu na kuwanyang'anya silaha wanamgambo mafisadi ambao si sehemu ya vikosi vya ulinzi."
Vikosi maalumu vya polisi vitavaa sare mpya ambazo zitawatofautisha na vikosi vyengine vya polisi, na wamechaguliwa kulingana na vigezo na ujuzi maalumu, kwa vile wao wanachukuliwa kuwa ni kikosi cha uingiliaji kati kwa haraka, alisema Abukar Dahir Osman, katibu mkuu katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa.
"Tutahakikisha kutoa magari maalumu ya doria kwa ajili ya kikosi cha silaha cha polis pamoja na simu na vifaa vya tahadhari na mfumo wa usimakizi katika vitongoji vyote vya mji mkuu," aliiambia Sabahi. "Magari haya yatakuwa yameundwa maalumu kwa ajili ya polisi kwa vile yatakuwa vyombo vinavyotembea kwa maringi yote manne vyenye uwezo wa kuwakimbiza wanamgambo katika barabara za mchanga."
Alisema kuwa serikali itapaswa pia kusimamia mawasiliano ya simu ili kuwatambua wanamgambo washukiwa na kukusanya habari za kiintelijensia kuhusu mashambulizi yoyote yaliyopangwa.
"Tunaona kwamba kulikuwa na mawasiliano baina ya mmoja wa mlipuaji wa bomu la kujitoa muhanga na kiongozi wa al-Shabaab baada ya walipuaji wanane wa mabomu ya kujitoa muhanga walipolilenga jengo la mahakama la Benadir hapo tarehe 14 Aprili," Osman alisema. "Kwa sababu hii, tunahitaji kuwa na teknolojia ya kisasa kabisa mkononi mwetu na zana za ulinzi ili kukwamisha mipango, matumaini na operesheni mbaya zinazotekelezwa na walipuaji mabomu wa kujitoa muhanga."
Serikali ya Somalia yatafuta msaada wa kimataifa
Mohamed alisema kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa itaziomba Marekani, Uingereza, China pamoja na nchi nyengine za Kiarabu, Kiafrika na Ulaya kwa ajili ya msaada wa vifaa vya kukipatia zana kitengo cha polisi pamoja na magari na helikopta.
Baadhi ya nchi tayari zimeshaahidi kutoa huduma za kijeshi, kipolisi na kiusalama pamoja na zana za kijeshi ili kusaidia kuuzuia mtandao wa al-Qaida na wa waashirika wake wa Somalia wasipange mashambulizi ya kigaidi, alisema.
Mwezi wa Aprili, serikali ya Djibouti ilitoa msaada wa magari ya kivita 15 kama sehemu ya sherehe ya kuhitimu kwa maafisa 205 wa Somalia waliomaliza kozi ya mafunzo ya usalama uliyoendeshwa na Ulaya nchini Djibouti, na inapanga kutoa msaada wa magari mengine.
Somalia inahitaji msaada kamili wa jumuiya ya kimataifa ili kuendesha operesheni za kupambana na ugaidi mjini Mogadishu, alisema Abdirashid Enow Nur, mchambuzi wa masuala ya kiusalama na profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Mogadishu. Vyenginevyo, mji mkuu utakuwa katika hatari ya mashambulizi ya al-Shabaab, alisema.
"Mogadishu bado milango yake iko wazi kwa wale wanaotaka kutega mabomu na kusababisha maafa bila ya upinzani wowote," Nur aliiambia Sabahi.
"Kwa hivyo, serikali lazima iharakishe na kunyanyua vikwazo vya ardhini vya kulinda milango ya kuingilia ya kaskazini na kusini ili kudhibiti hali ya usalama," alisema. "Kwa kuongezea, inapaswa kutumia mbwa wa polisi waliopewa mafunzo ili kusaidia kugundua milipuko na madawa katika vituo vya upekuzi vya kuingilia na mipakani kwa sababu hao wanafaa zaidi kuliko vifaa vya ukaguzi kwa kutumia mikono na kwa sababu ni kipaumbele cha juu katika kazi ya usalama."
Chanzo: sabahionline.com



No comments:
Post a Comment