Na Abdi Said, Mogadishu
Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) imefungua kliniki za afya nane na hospitali tatu katika maeneo yaliyokombolewa kutoka kwa al-Shabaab, kwa mujibu wa msemaji wa AMISOM Kanali Ali Aden Humad.

Wakina mama na watoto wakisubiri huduma za matibabu kwenye kituo cha jeshi cha AMISOM huko Halane jijini Mogadishu. [Abdi Said/Sabahi]
Kliniki hizo zipo katika wilaya kadhaa za mikoa ya Shabelle ya Kati na ya Chini, na hospitali hizo zipo Beledweyne, Kismayo na Baidoa. Zinatoa huduma kamili mbalimbali za afya, Humad alisema.
"Tuna vifaa vya kisasa vya huduma za afya, ikiwa ni pamoja na vifaa vya maabara kwa ajili ya kuchunguza magonjwa ya kawaida, mashine ya kufanya eksirei kwa jeraha ya mfupa, mashine ya kuchunguza shinikizo juu la damu na kisukari, na dawa hutolewa bure na madaktari wenye sifa za hali ya juu," aliiambia Sabahi.
AMISOM imeweka katika hospitali hizo madaktari wawili na wauguzi kumi kwa kila moja ili kuhudumia wagonjwa wapatao 300 kwa siku. Vituo vidogo vya afya huhudumia wagonjwa wachache, Humad alisema. Kliniki jongevu za afya pia zipo na zinatoa huduma vijijini.

Abdi Malim Hussein, mwenye umri wa miaka 12, akipata huduma za matibabu katika hospitali ya AMISOM jijini Mogadishu. Hussein alipigwa risasi kwenye nyonga mwezi Machi na al-Shabaab baada ya yeye na marafiki zake wanne kujaribu kutoroka kwenye kambi ya mafunzo katika wilaya ya Mahadey huko Shabelle ya Kati mahali walipopelekwa na kushikiliwa mateka. [Abdi Said/Sabahi]
AMISOM ilifungua vituo hivyo baada ya kushauriana na wazee wa kimila, ambao waliwaambia kwamba huduma za afya miongoni mwa watu zinahitajika sana. Gharama za uendeshaji zinatoka moja kwa moja kwenye bajeti ya AMISOM.
Vituo vya afya vinasaidia kutimiza ahadi ya Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ya kutoa msaada wa kiafya kwa maeneo yaliyokombolewa kutoka kwa al-Shabaab, alisema Humad. "[AMISOM] itaendelea kutoa huduma hizi hadi uwezo wa serikali utakapoongezeka [na kuchukua usimamizi]," alisema.
Wasomali wamepongeza kurejea kwa mashirika ya kutoa misaada katika maeneo ambayo awali yalidhibitiwa na al-Shabaab, ambao walizuia mashirika ya kutoa misaada kuingia na kuwaweka watu walio katika mazingira magumu hatarini.
Wakati wa msimu wa mvua mwezi Machi, vituo vya AMISOM vilitoa matibabu ya haraka, ambayo awali hayakupatikana kwa wananchi 600 walioathiriwa na mlipuko wa kipindupindu huko Beledweyne.
Wagonjwa walihamishiwa katika vituo vipya viwili vya afya vya AMISOM vilivyofunguliwa huko El Jalle na kupata matibabu papo hapo, jambo ambalo lilisaidia kutosambaa kwa ugonjwa, mmoja wa timu ya tiba ya AMISOM Daktari Abdi Gedi Warfa aliiambia Sabahi.
Safiya Farah, mama wa watoto watano mwenye umri wa miaka 34, alisema vituo vya El Jalle vilisaidia kuwahudumia watoto wake wawili.
"Niligundua kwamba kipindupindu kilikuwa kikisambaa na kwamba sikuwa na mahali pa kupeleka watoto wangu, [lakini cha kushukuru] tumepokea msaada kutoka AMISOM," aliiambia Sabahi. "Sikuwahi kufikiria ningepata msaada huo kutoka kwa vikosi vya AMISOM. Sasa watoto wote wana afya na ninashukuru kwa ndugu zetu wa AMISOM kwa jitihada walizozifanya kwa niaba yetu."
Mariam Hirsi, mama wa watoto watatu mwenye umri wa miaka 35 katika wilaya ya Lego huko Shebelle ya Chini, alisema kupatikana kwa huduma ya afya kumepunguza hofu yake ya gharama za matibabu.
"Awali nilikuwa nikihofu sana kuhusu fedha nilizotumia katika uchunguzi wa afya, lakini sasa, ninamshukuru Mungu, tumepata huduma za bure za afya kwa ajili ya watoto wetu na Mungu amewaondoa al-Shabaab waliokuwa wakitutawala," aliiambia Sabahi.
Ali Yusuf, mzee wa kimila mwenye umri wa miaka 55 huko Baidoa, alisema vituo vya afya vinaakisi matakwa ya AMISOM kuwasaidia watu wa Somalia.
"Wakati wa utawala wa al-Shabaab, wakaazi wa Baidoa walikandamizwa katika njia nyingi ambazo zilitishia maisha yao na ilikuwa vigumu kwao kupata huduma za bure za afya," aliiambia Sabahi. "Lakini leo, wakaazi wa Baidoa wameelewa anayeendeleza na asiyeendeleza maslahi yao."
Chanzo: sabahionline.com



No comments:
Post a Comment