Na Victor Melkizedeck Abuso
Marekani inasema itachukua hatua dhidi ya Syria baada ya kutokea kwa shambulizi la silaha za kemikali wiki iliyopita jijini Damascus na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa Mambo ya nje John Kerry amesema kuwa kilichotokea nchini Syria hakikubaliki kamwe na ni lazima serikali ya rais Bashar Al Assad iwajibike kwa mauaji hayo.
Marekani na washirika wake kama Ufaransa na Uingereza wanasema wakati umefika kwa Syria kuvamiwa kijeshi pendekezo ambalo washirika wa karibu wa rais Assad China na Urusi wanapinga.
Leo ni siku ya pili ya uchunguzi unaofanywa na watalaam wa Umoja wa Mataifa kubaini ikiwa kweli silaha za kemikali zilitumiwa dhidi ya raia wasiokuwa na wakati.
Rais Bashar Al Assad amesema kuwa tishio la Marekani kuwa ikiwa uchunguzi utabaini kuwa silaha hizo zilitumiwa, italazimika kuingilia mzozo huo kijeshi ni jambo ambalo halikubaliki kamwe.
Akihojiwa na gazeti la kila siku la Urusi la Izvestia Assad amesisitiza kuwa Marekani haitafaulu na kamwe hawezi kuwa kibaraka cha mataifa ya Magharibi na ataendelea kupambana na makundi ya kigaidi yanayolenga kuiangusha nchi yake.
Mwaka uliopita, rais Obama alionya kuwa ikiwa serikali ya Syria itatumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani , nchi yake itaivamia kijeshi.
Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza William Hague naye amesema kuwa ikiwa silaha hizo zilitumiwa ni sharti hatua zichukuliwe lakini anahofia kuwa huenda ushahidi wa kufahamu ukweli umeshaharibiwa.
Serikali ya Assad imeendelea kusisitiza kuwa haiwezi na haijawahi kutumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani na itafanya hivyo ikiwa nchi yake itavamiwa na watu kutoka nje.
Machafuko nchini Syria yamesabisha zaidi ya watu Laki Moja kupoteza maisha kwa kipindi cha miaka miwli iliyopita kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, na Mamilioni kusalia kuwa wakimbizi wakiwemo watoto.
Suluhu ya mzozo wa Syria inasalia kuwa kitendawili baada ya juhudi za Kidiplomasia kugonga mwamba.
Via kiswahili.rfi.fr
Via kiswahili.rfi.fr



No comments:
Post a Comment