Na Bosire Boniface, Garissa
Utulivu wa kiasi umerejea baina ya jamii za Gabra na Borana kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia baada ya kuibuka kwa wasiwasi wa kisiasa uliovuma wiki iliyopita, ukisababisha watu wapatao 12 kupoteza maisha na zaidi ya 60,000 kukosa makazi.

Mwonekano wa Moyale, mji ulio mpakani ambao uko kando kando ya Kenya na Ethiopia, tarehe 22 Agosti, Vurugu baina ya makabila ya Gabra na Borana katika wiki za hivi karibuni ziliwaua watu wapatao 12 na zaidi ya 60,000 kukosa makazi. [Bosire Boniface/Sabahi]
Kuibuka kwa vurugu wa hivi karibuni kulianza tarehe 22 Agosti wakati watu watatu walipouawa huko Marsabit, na dereva wa lori kushambuliwa kwenye njia kubwa ya magari itokayo Nairobi kwenda Moyale. Siku mbili baadaye, watu wengine watatu waliuawa katika mapigano ya vita vidogo baina ya jamii za Borana huko Moyale.
Kati ya tarehe 29 na 30, watu sita zaidi waliuawa na zaidi ya watu 20,000 walikimbia katika mpaka huo kuingia Ethiopia, ambayo iko umbali wa chini ya kilometa moja kutoka mji wa Moyale, Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya Stephen Bunaya aliiambia Sabahi.
"Takribani watu wengine 40,000 wanapiga kambi ndani ya shule nchini Kenya," alisema. "Shule zimefungwa na wakati zitakapofungiuliwa familia hizo zitapaswa kuondoka."

Umbali kutoka Moyale nchini Kenya na Ethiopia ni chini ya kilometa moja. [Bosire Boniface/Sabahi]
Wakati wa vurugu, Bunaya alisema nyumba zaidi ya 50 yakiwemo majengo ya biashara yalichomwa moto.
Mzozo baina ya jamii hizi mbili ni wa kawaida na aghalabu husababishwa na siasa na ulipizaji kisasi, alisema Ali Abdi, mwandishi wa habari mwenye makazi huko Isiolo ambaye anajua vema mapambano hayo.
Waborana ndiyo walio wengi katika wilaya ya Moyale, wakati Gabra ndiyo walio wengi katika maeneo ya jirani ya wilaya ya Marsabit. Katika uchaguzi mkuu wa tarehe 4 Machi, Gabra walichukua viti vyote vya juu vya kaunti na kusababisha maoni ya chinichini ya kutoridhika miongoni mwa Wabarona, Abdi alieleza.
"Kumekuwa na hisia miongoni mwa Waborana katika Kaunti ya Marsabit kwamba walipaswa kuwa na angalau viongozi wawili katika viti vya juu vya kaunti ili kuhakikisha wanawakilishwa vya kutosha," aliiambia Sabahi.
Hatua ya serikali ya taifa na ya kaunti kuwahamishia familia za Gabra karibu na Sololo mwezi Julai ilichochea vurugu ambazo zilizuka katikati ya Agosti, Abdi alisema.
"Waborana walipinga hatua hiyo wakidai eneo ni ardhi ya mababu zao na familia za Gabra zimeletwa humo kutoka Ethiopia," alisema. "Kulikuwa na shambulizi katika familia zilizohamishiwa hapo na kilichofuatia ni ulipizaji kisasi."
Hali hiyo iliendelea wakati wazee wa ukoo wa jamii mbili ambao wanaishi Ethiopia walipojihusisha. "Kulikuwa na malalamiko ya kisiasa, lakini kupewa makazi kwa familia za Gabra ulichochea vurugu," Abdi alisema.
Wakaazi waomba amani
Wakaazi waliozungumza na Sabahi walisema hali sasa imetulia, lakini kulikuwa na wasiwasi wa chinichini.
"Kwa sasa hali imetulia kwa sababu maofisa usalama wako katika doria lakini hakuna walio tayari kurudi kwenye nyumba zao kwa kuhofia uwezekano wa kushambuliwa," alisema Huka Hassan Ali, Mgabra mwenye miaka 34 mkaazi wa kitongoji cha Funyatta.
"Washambuliaji walikuja kwetu na kutuambia tuhame katika ardhi hiyo kwa sababu ni mali ya kabila la Borana," alisema. "Ninaamini wanasiasa wa Borana walihuisika na mashambulio haya kwa sababu kulikuwa na mazungumzo kwamba kabila la Gabra wasitarajie kuishi katika ardhi ya Borana kama hawatawaunga mkono viongozi wao."
Alisema ugomvi umekuwa ukiathiri biashara zote. "Tunataka tu utulivu urejee ili tuweze [kulisha] kwa familia zetu," alisema. "Nimekuwa nikiona inatosha kwa ugomvi kusababishwa na tofauti zetu za kisiasa."
Abdi Golicha, mwenye umri wa miaka 37, wa kitongoji cha Odda, alisema vurugu hiyo ilisababisha kifo cha binamu yake.
"Mimi ni wa kabila la Borana lakini vurugu ziliniacha na msiba," alisema. "Vurugu hizo zinatufundisha kwamba hakuna mwenye mamlaka ya kufanya vurugu. Tunapaswa kuishi kwa utulivu na kuzika tofauti zetu. Nimeumizwa na msiba, lakini sina mpango wa kulipiza kisasi chochote kwa ajili ya amani."
Serikali ya Kaunti yaahidi kuwa jumuishi
Katika ahadi ya kuzuia vurugu zisienee katika miji mingine, serikali siku ya Alhamisi (tarehe 29 Agosti) ilipeleka vikosi zaidi vya usalama katika mkoa huo, ikiwa ni pamoja na jeshi, Kamishna wa Kaunti ya Marsabit Isaiah Nakoru aliiambia Sabahi.
"Tunazuia utokeaji kutokana na somo lililopita ambapo shambulio kati ya jamii mbili lilisambaa katika miji mingine kama Marsabit," alisema. "Tunafanya pia usindikizaji wa kiusalama kwa wenye magari."
Nakoru alisema wanafanya kazi pamoja na mamlaka za Ethiopia kudhibiti makabila yanayopigana pande zote za mipaka. Hadi sasa, maofisa wa Kenya wa eneo hilo wamewakamata watu wapatao 40 na wanawahoji baadhi ya viongozi wa jamii kujua ushiriki wao katika vurugu za hivi karibuni, alisema.
Gavana wa Kaunti ya Marsabit Ukur Yatani alisema kwamba viongozi kutoka katika jamii hizo mbili wametoa wito kwa ajili ya kusitisha mapigano wakati wakitafuta suluhisho la vurugu hizo.
"Vurugu lilikuwa ni jambo la mwisho tulilotarajia tulivyokuwa tukiandaa kutekeleza miradi ya maendeleo," aliiambia Sabahi. "Tulipokea tu sehemu yetu ya fedha kutoka katika serikali ya taifa na hatutawavumilia wanaoanzisha vurugu kwa ajili ya kufuta maendeleo."
Zaidi ya makabila ya Borana na Gabra, kuna makabila ya Burji, Wasomali, Gare na makabila madogo ambayo yote yatakuwa na sehemu yao katika maendeleo, alisema.
"Katika mifumo iliyopita kulikuwa hakuna usawa katika mgawanyo wa rasilimali na kazi, lakini chini ya usimamizi wangu hakuna hata mmoja atakayehisi ameachwa nje," alisema.
Chanzo - sabahionline.com



No comments:
Post a Comment