If you need it, we can provide: • USA 24 hours Passport service • Rush and emergency USA passport • Expedited Visa process for U.S. & foreign countries • Document Authentication •Document Legalization..For more information please contact us at: 703-286-7713

http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.htmlKwa kuchangia chochote kile alichonacho kupitia Hilmy Disability Charity Organisation. Wasiliana na Mkurugezi wa Hilmy Disability Charity Organisation. Faria Zam. kwa UK Number ya Simu. 745-501-4372 Au Abou Shatry. U.S.A No' 301-728-3977

 http://www.dickysmallsauto.com/

DICK SMALLS AUTO MOTIVE WE CAN HANDLE ALL OF YOUR REPAIR AND SERVICE NEEDS INCLUDING CALL US NOW!(301) 931-3300. 10111B BACOCON DRIVE,BELTSVILLE,MD 20705


Sunday, October 13, 2013

Ahadi ya Tanzania ya uhuru wa vyombo vya habari yatiliwa shaka baada ya kufungwa kwa magazeti

Na Deodatus Balile, Dar es Salaam

Uamuzi wa hivi karibuni wa serikali ya Tanzania kusimamisha kwa muda uchapishaji wa magazeti mawili ya kila siku unadhoofisha kanuni ya utawala bora na kuharibu sifa ya Tanzania nchi za nje, wataalamu wa vyombo vya habari na wataalamu wa sheria wanasema.

Watu wakisoma vichwa vya habari vya gazeti katika pahali pa kuuzia magazeti huko Dar es Salaam tarehe 28 Septemba, siku moja baada ya serikali kutangaza kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania. [Deodatus Balile/Sabahi]

Kuanzia tarehe 27 Septemba, Mwananchi lilifungiwa kwa siku 14 na Mtanzania kwa siku 90 kwa tuhuma za kuchapisha makala za uchochezi ambazo serikali ilisema zinatishia usalama wa taifa na kuvunja amani na mshikamano katika nchi.

Serikali ilitumia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kuyazuia magazeti hayo kuchapishwa.

Mwanasheria Nyaronyo Mwita Kichere alisema sheria ilipaswa kuwa imebatilishwa mwaka 1992, wakati ilipojumuishwa kwenye orodha ya sheria 40 zilizopendekezwa kubatilishwa na Tume ya Nyalali, ambaye wakati huo alikuwa Jaji Mkuu Francis Nyalali.

"Sheria hii inatoa madaraka ya kipekee katika mikono ya waziri mmoja, ambaye anaweza kufanya uamuzi wa kufungia gazeti bila ya kuwapa wamiliki au wahariri husika fursa ya kusikilizwa," Kichere alisema. "Ni sheria mbaya kwa vigezo vyote."

Tanzania ilitia saini katika Ushirikiano wa Uwazi wa Serikali, ambao unataka kwamba serikali ziwe wazi kwa raia katika kila kitu zinachokifanya, alisema.



Makala ambazo zilisababisha kufungwa zilikuwa habari za Mwananchi kuhusu mishahara ya serikali ambayo ilijikita katika nyaraka za siri, na makala ya Mtanzania kilichokuwa na kichwa cha habari "Waislamu waabudu chini ya ulinzi mkali" ambacho kilitumia picha ya mbwa wa polisi wa serikali, ambayo kwa kiasi ilionyesha serikali ilikuwa ikipeleka mbwa katika miskiti.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vyombo vya Habari la Tanzania Kajubi Mukajanga alisema kufungwa kwa gazeti kunadhoofisha demokrasia.

"Hatua zilizochukuliwa na serikali ni za kusikitisha na sio za kidemokrasia na kuipeleka nchi muongo mmoja nyuma katika jitihada za kujenga jamii ya kidemokrasia ambayo inaheshimu uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari," Mukajanga aliiambia Sabahi.

Uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi zaidi ambayo inainua haki za wengine kutambuliwa, alisema akiongeza kwamba Tanzania inapaswa kujitahidi kuulinda kwanza na kuupa umuhimu.

Siku ya Jumatano (tarehe 9 Oktoba), wadau kutoka vyombo huru vya habari vya Tanzania waliandamana kutokana na kufungiwa hivi karibuni na kutoa tamko lililotangaza mgomo usiokuwa na mwisho wa habari zinazohusiana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fenella Mkangala na Mkurugenzi wa Huduma za Habari Tanzania Assah Andrew Mwambene.

Sio mara ya kwanza
Mwananchi na Mtanzania sio magazeti ya kwanza ambayo serikali imeyafunga hivi karibuni.

MwanaHalisi, gazeti la kiuchunguzi linalotoka kila wiki, lilifungiwa kabisa mwezi Julai 2012 kwa kuchapisha kile serikali ilichokiita "habari za uchochezi na za uongo".

Katika toleo lake la mwezi Julai, MwanaHalisi lilichapisha mfululizo wa makala kuhusu shambulizi la mwishoni mwa Juni dhidi ya Stephen Ulimboka, mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania.

Ulimboka aliongoza maandamano katika mvutano baina ya serikali ma madaktari kuhusu ongezeko la mishahara wakati alipotoroshwa na kuteswa.

MwanaHalisi iliripoti kwamba ofisa wa usalama wa taifa wa Ikulu alituhumiwa kula njama na watu wengine watatu katika shambulizi dhidi ya Ulimboka. Gazeti pia lilichapisha namba za simu za wale linalodai walikuwa wakosaji wa shambulizi, likionyesha muda na mahali ambapo simu zilipigwa kwa tuhuma ya kupanga utoroshaji.

"Kama tulichokichapisha kuhusu washambuliaji ni uongo, fikra zangu zinanieleza kwamba serikali ilibidi ije na toleo sahihi ambalo linaviondoa lawamani vyombo vya dola," alisema Saed Kubenea, mmiliki na mhariri mkuu wa MwanaHalisi.

"Ukimya wa serikali ni kukiri kwamba vyombo vyake vilihusika katika shambulizi kwa namna moja au nyingine," aliiambia Sabahi.

Baada ya MwanaHalisi kuandika mfululizo huo, serikali mara moja ilikana kuhusika kwa ofisa wa usalama wa taifa na kusema habari hizo zina tuhuma zisizo na msingi zikidhamiria kuusisimua na kuuchochea umma.

Raia wa Kenya Joshua Murundi alikamatwa kwa shambulizi hilo na kushtakiwa kwa kosa katika Mahakama ya Kisutu mwezi Septemba 2013. Mahakama ilimuhukumu kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya shilingi 1,000 (dola 0.62).

Murundi alilipa faini na sasa yuko huru.

Hapo awali serikali ilitumia Sheria ya Magazeti kulifungia MwanaHalisi mwezi Oktoba 2008 kwa miezi mitatu kuhusiana na makala zilizochukuliwa kuwa za uchochezi na kumkashifu rais, kwa mujibu wa Kamati ya Kuwalinda Waandishi (CPJ).

Kubatilisha Sheria ya Magazeti ya 1976
Absalom Kibanda, mhariri mtendaji wa gazeti la Mtanzania, alisimamia stori yake ya gazeti, lakini alisema kwamba hata kama gazeti lilifanya makosa, adhabu ilikuwa kali mno.

"Kulifungia gazeti hakukubaliki, lakini pia kulifungia kwa siku 90 ni kitu ambacho sikuwahi kufikiria." aliiambia Sabahi. "Sheria iliyotumika ni mbaya na watunga sheria wanapaswa kutazama uwezekano wa kuibatilisha haraka iwezekanavyo."

Tarehe 6 Oktoba, kaimu kiongozi wa upinzani Zitto Kabwe alitoa tamko katika vyombo vya habari akisema alikuwa amewasilisha mswada kwa katibu wa Bunge la Taifa akiomba kuibatilisha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.

Jukwaa la Wahariri wa Tanzania, mashirika mbalimbali ya vyombo vya habari vya kimataifa na baadhi ya wanasiasa pia walitoa matamko wakilaumu serikali kwa ajili ya kufungwa na kuwaomba watunga sheria kuibatilisha sheria hiyo.

"Serikali ilipaswa kupeleka malalamiko yake dhidi ya Mwananchi na Mtanzania katika Baraza la Vyombo vya Habari Tanzania, badala ya kuyasimamisha katika uchapishaji," alisema Mshauri wa CPJ Afrika Mashariki Tom Rhodes. "Tunatoa wito kwa mamlaka kuruhusu urejeshaji wa uchapishaji na kufanya mabadiliko ya sheria ambazo zinaruhusu usimamishaji huu, ambao hauendani na viwango vya kimataifa vya uhuru wa vyombo vya habari."

Neville Meena, mhariri wa Mwananchi na katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, alikiri kwamba wahariri wa gazeti walikuwa wakiangalia uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya serikali.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma za Habari Tanzania Assah Mwambene alitetea uamuzi wa serikali na kusema mamlaka hazikuchukua hatua nje ya sheria lakini badala yake zilifuata hatua zote.

"Tuliyaonya [magazeti] mara nyingi," Mwambene aliiambia Sabahi. "Kwa gazeti la Mtanzania tuliwataka kuwasilisha majina ya wahariri wenye sifa kwa sababu aliyesababisha matatizo hakuwahi kupata mafunzo ya uandishi wa habari, lakini hawakutekeleza. Kwa hiyo, kwa sababu ya usalama, tulilazimika kuchukua hatua hizi."

Mwambene alisema kwamba kama waandishi wa habari watafuata maadili ya vyombo vya habari na kueleza ukweli, hakutakuwa na tatizo.

Chanzo - sabahionline.com

No comments:

Post a Comment

Maoni yako