Na Ali Adam, Mogadishu
Furaha zilitanda katika mitaa ya Mogadishu Jumanne (tarehe 15 Oktoba) kwani makundi ya Wasomali waliungana na Waislamu duniani kote kuadhimisha siku ya kwanza ya Eid al-Adha.

Wavulana wa Somalia wakicheza mieleka katika mchanga kwenye ufukwe wa Lido huko Mogadishu kusherehekea Eid al-Adha. [Ali Adam/Sabahi]
Mamia ya waumini walishangilia kwa kukusanyika katika msikiti wa Isbahaysiga huko Mogadishu kuswali, ikiwa ni pamoja na Rais Hassan Sheikh Mohamud na maofisa wengine wa nchi.
Mohamud alihutubia mkusanyiko wa waumini baada ya swala ya Eid, akituma salamu za sikukuu kwa watu wa Somalia walio nyumbani na nje ya nchi akiwatakia amani na maendeleo.
Rais pia alijadili hali ya usalama na kisiasa ya nchi, na kutoa wito kwa wanachama wa al-Shabaab kukumbatia amani na kujitoa katika shughuli za kigaidi.
"Ninawaambia vijana ambao ni sehemu ya al-Shabaab, rudini kwa watu wenu na nchi yenu kwani hamna watu wengine nje ya watu wenu. Wakati mtakaporudi kwa watu wenu kwa majuto makubwa na kuacha kusababisha matatizo, watawasamehe," Mohamud alisema

Watoto wa Somalia wakiwa kwenye ufukwe wa Lido wakati wakisherehekea Eid al-Adha na familia zao [Ali Adam/Sabahi]
Kufuatia swala ya Eid, familia zilizovalia vizuri ziliingia katika mitaa ya mji mkuu wa Somalia kushangilia na ndugu na marafiki.
Elmi Mohamed, mwenye umri wa miaka 37, ambaye alirejea nyumbani kutoka Sweden miezi miwili iliyopita, alisema alihisi kuwa yeye ni mwenye bahati kusherekea sikukuu ya Eid nyumbani huko Mogadishu.
"Nina hisia sana leo kwa sababu ninasherehekea Eid katika Mogadishu ya amani," aliiambia Sabahi. "Hiyo ni furaha isiyosahaulika na ninawatakia Wasomali wote popote walipo Eid njema."
Kutoa kwa wasio na uwezo
Eid al-Adha ni sikukuu kubwa katika kalenda ya Kiislamu. Wakati wa siku nne za kusherehekea, Waislamu huchinja wanyama na kutoa baadhi ya nyama kwa wasiokuwa nacho katika jamii.
Katika kuendeleza desturi hii, Chama cha Hilali Nyekundu cha Falme za Kiarabu kilichinja wanyama wengi katika viunga vya Tarabuunka katika wilaya ya Hodan huko Mogadishu, makazi ya kambi kubwa za watu wasiokuwa na makazi nchini.
Halima Ibrahim, mkaazi wa kambi ya Zone K ,mwenye umri wa miaka 36, aliiambia Sabahi kwamba hata kama maskini hawawezi kumudu kununua nguo mpya kwa ajili ya watoto wao, walikuwa wakiungana na ndugu zao ambao ni matajiri huko Mogadishu kusherehekea Eid.
"Ninawashukuru ndugu zetu waliotupatia zawadi hii kwa kuchinja wanyama kwa ajili yetu. Mungu aliipanga, tumekula nyama nyingi leo," alisema.
Kwingine mjini, familia na vijana walijaa katika Ufukwe wa Lido na maeneo mengine ya baharini kufurahia sikukuu.
Kwa Habiba Roble, mwenye umri wa miaka 41, ilikuwani mara yake ya kwanza kusherehekea Eid al-Adha akiwa nyumbani baada ya kuishi nje ya nchi kwa miaka saba.
"Siwezi kusema ni jinsi gani nilivyo na furaha sasa kwamba nipo katika Ufukwe wa Lido," Roble aliiambia Sabahi. "Nimeishi katika Jamhuri ya Falme za Kiarabu kwa muda na sijawahi kusherehekea kama hivi. Leo ninafurahia mwenyewe katika nchi yangu."
Wakati huo huo, watoto walionekana wakicheza na vitu vya kuchezea mitaani. Baadhi yao, ikiwa ni pamoja na Musab Abdirahman mwenye umri wa miaka 8, walicheza karibu na Sanamu ya Ukumbusho ya Mwanajeshi asiyetambulika katika wilaya ya Bondhere huko Mogadishu.
"Ninacheza pamoja na watoto wengine kutoka katika kitongoji changu wakati sikukuu ya Eid al-Adha ikiendelea," alisema. "Baba yangu alininunulia nguo, viatu na kila kitu."
Chanzo: sabahionline.com



No comments:
Post a Comment