BY RAPHAEL KIBIRITI
Wasomi na wanaharakati wametoa maoni tofauti kufuatia tangazo lililotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi kuwa,wabunge wake wanaingia katika Bunge Maalumu la Katiba na ajenda ya kulinda na kutetea muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Mhadhiri toka katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwalimu Bashiru Ally amesema, kimsingi mchakato mzima kuhusiana na suala hili la kupata katiba mpya ulikosewa toka mwanzo.
“Kwa kuwa muungano wetu ni wa nchi mbili zenye ukubwa tofauti lakini zilizo na hadhi sawa, tulipaswa kuwa na mjadala wa kitaifa kama maandalizi, kabla hata ya kuundwa kwa Tume ya Jaji Warioba ili tufikie maridhiano na maafikiano ya namna ya kuushughulikia mchakato huu,” alisema.
Alisema endapo hilo lingefanyika, kusingekuwa na haja ya wajumbe wa kuingia kwenye bunge maalumu kupatikana kwa kuteuliwa kama ilivyokuwa sasa, bali wangepatikana kwa kupigiwa kura na wananchi, hali ambayo ingewahakikishia maslahi yao.
Hata hivyo mwalimu Ally aliwaasa wananchi kuondokana na mawazo potofu kwamba, kitendo cha CCM kuwa na wajumbe wengi kwenye bunge maalumu la katiba, ni tiketi ya kupata katiba mbaya.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Deus Kibamba alitofautiana na msimamo huo wa CCM, akisema kitendo hicho cha kutoa maelekezo kwa wabunge wake wachukue msimamo fulani wa kichama ni cha kulivuruga bunge maalumu kabla hata halijaanza.
“Ingawaje CCM kama kundi lingine ina haki ya kutoa hoja na kushauri chochote, lakini kinapaswa kujua kwamba bunge maalumu haliendeshwi kama bunge la kawaida, ambalo huongozwa na itikadi za kivyama,” alisema.
Kibamba alisema, ni kwenye bunge la kawaida ndiyo kunakuwa na wabunge wa chama tawala kulia na wa upinzani kushoto.
Alisema, bunge la katiba liko kwa ajili ya kutafuta muafaka wa nchi na hivyo wajumbe wake wanatakiwa waongozwe na hoja zenye tija, zitakazofanya wajumbe wengine wazione na kukubaliana nazo na siyo suala la wengi wape, kama ilivyo kwenye bunge la kawaida.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema, si sawa kwa CCM kushinikiza wabunge wake wakasimamie wapi kwenye bunge maalumu la katiba.
Mhadhiri wa Chuo cha Mipango na Maendeleo vijijini, Lawrence Buguzo, alisema kuwa tatizo ni kuchanganya katiba ya chama na ya nchi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataalum katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Paul Loisulie, alisema inawezekana misimamo ya vyama ikawa katika pande mbili, lakini pia kwenda na msimamo ni jambo zuri ingawa ukiangalia kwa upande mwingine siyo zuri.
SOURCE: NIPASHE



No comments:
Post a Comment