Sunday, June 19, 2016

KENYA: WABUNGE WA CORD PIA WAMPA MSAMAHA KURIA

Na CHARLES WASONGA

MUDA mfupi baada ya kiongozi wa Cord Raila Odinga kutangaza kuwa amemsamehe Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, viongozi wengine walioshtakiwa kwa tuhuna za kuchochea chuki pia walisema wamemsamehe.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria. Picha/MAKTABA

Akiongea kwa niaba yao, Seneta wa Machakos Johnstone Muthama alisema wao pia wamemsamehe Bw Kuria bila masharti yoyote.

“Kwa sababu kiongozi wetu Mheshimiwa Raila Odinga ametangaza kuwa amemsamehe ndugu yangu hapa ambaye ndiye aliyepelekea majina yetu kuwekwa kwenye hati ya mashtaka, mimi pamoja na wenzangu hapa pia tunamsamehe bila masharti yoyote,” akasema kwenye video iliyonaswa Alhamisi katika seli za Mahakama ya Milimani, Nairobi.

Muthama alisema hayo kwa niaba ya wabunge wa Cord Junet Mohammed (Suna Mashariki), Florence Mutua (Busia), Timothy Bosire (Kitutu Masaba) na Aisha Jumwa (Kilifi) ambao walishtakiwa kwa kujibu Kuria aliyedaiwa kusema kuwa Bw Odinga anafaa kuuawa.

Video hiyo ambayo ilisambazwa jana ilienezwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha Kuria, Muthama na wakili James Orengo wakihojiwa na wanahabari katika seli za chini kwa chini katika mahakama hiyo.


Naye Kuria akijibu kuwa kusema: “Nadhani tukio hili limetuonyesha kuwa shida zetu ni ndogo sana kuliko shida za taifa hili. Mimi na ndugu yangu hapa (Muthama) tumefanya kazi nyingi pamoja na sidhani kuwa mambo madogo kama haya yanaweza kututenganisha”

Kwa upande wake Bw Orengo ambaye pia ni Seneta wa Siaya alisema madhila ambayo wabunge hao, wakiwemo Kimani Ngunjiri (Bahati) na Ferdinand Waititu (Kabete), walipitia katika seli siku nne ni msingi wa kufanya kazi pamoja.

“Tumegundua kuwa Kenya ni kubwa kuliko sisi. Ninaamini kuwa tunaweza kufanya kazi pamoja kwa minajili ya kupalilia uthabiti na maendeleo katika taifa hili,” akasema Bw Orengo.

Akaongeza: “Sikujua kuwa ndugu yangu Kuria anaweza kuongea Kiarabu. Nakumbuka nilikutana naye Dar es saalam (Tanzania mwaka jana nilipokwenda kushangilia Gor Mahia nikagundua kuwa ni shabiki sugu wa timu hiyo.”

Bw Kuria alisema atamtembelea Orengo nyumbani kwake Ugenya kuonyesha wakazi wa huko kuwa wameridhiana na kuamua kufanya kazi pamoja.

Baadaye wabunge hao walikumbatiana mbele ya kamera za wanahabari kuashiria kuwa wameridhiana.

Chanzo: swahilihub.com

No comments:

Post a Comment