Na Bosire Boniface, Garissa
Wakimbizi wa Somalia katika eneo la kambi ya wakimbizi ya Dadaab, wamesema wanatamani kurudi nyumbani, lakini wengi wao hawana uhakika na hali ya usalama katika maeneo yaliyokombolewa kutoka kwa al-Shabaab.
Wakimbizi wa Somalia katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab wanahudhuria sherehe za kuadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani tarehe 20 Juni 2012. [Abdullahi Mire/AFP]Adan Hussein Abdi, mwenye umri wa miaka 46, mkimbizi katika kambi ya Dadaab, amesema anatamani kurudi nyumbani na kutamani kama angeweza kurudi nchini kwake kushuhudia tukio la kihistoria wakati Somalia inaunda serikali yake kuu ya kwanza kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20.
"Ni maisha magumu kuishi katika kambi. Uhuru wetu wa kutembea na haki nyingine zinabanwa. Mgawo wa chakula wanaopokea wakimbizi katika makambi haya umepunguzwa hasa na tunahofia misaada nayo inaweza kuisha kabisa," aliiambia Sabahi.
Kituo cha kugawanya chakula cha msaada kinatoa kilo tatu za mahindi, unga wa ngano, uji, na kikombe cha mafuta kwa kila wiki mbili, ambavyo ni nadra kutosheleza kulisha familia, alisema.
"Kwa sababu hizi na nyingine nyingi, tuna imani kuwa viongozi wapya watafanya kazi kwa maslahi ya Wasomali walio wengi hivyo kwamba baadhi yetu tunaweza kurudishwa nyumbani na kujenga tena maisha yetu," alisema.
Maulid Ali Osman, mkimbizi mwenye umri wa miaka 32 katika kambi ya Hagadera, alisema anawaonea wivu wakimbizi wa Sudani Kusini ambao wamekuwa wakirudishwa nyumbani kusaidia kujenga nchi yao kutoka ilipopata uhuru mwaka uliopita.
Osman aliiambia Sabahi kuwa anangojea muda atakaoweza kurudishwa nyumbani. "Wakimbizi wa kambi ya Sudani [Kusini] walitukuta hapa katika kambi hii na wameondoka wametuacha. Tunawatakia kila la heri na ninaomba tusiendelee kuwa hapa kwa muda mrefu," alisema.
Timira Abdi Ali, mwenye umri wa miaka 42 na mama wa watoto wanne, anasema alikimbilia Kenya wakati mvulana mmoja kijana alipojilipua katikati ya kundi la watu kwenye soko la nchini kwao mwaka 2009, likamuua mtoto wake wa kiume.
Ali, ambaye sasa anaishi kwenye kambi ya Ifo ndani ya maeneo ya Dadaab, anasema tukio hilo lilimwogopesha sana kiasi kwamba aliapa kutorejea nyumbani kamwe. Hata hivyo, kuimarika kwa ulinzi hivi karibuni nchini Somalia kunabadilisha msimamo wake, alisema.
"Watoto wangu bado wanaogopa kutokana na mauaji waliyoyaona, milio ya bunduki, milipuko na roketi za makombora zikirushwa nyumbani, lakini ninadhamiria kurudi nyumbani," alisema. Hata hivyo, Ali alisema ulinzi unapaswa kuhakikishwa kabla ya wakimbizi kurejea nyumbani.
Kukosa matumaini ya ulinzi kunaendelea
Baadhi ya wakimbizi wanasema wamekaa muda mrefu na waliporudi nyumbani walikuta mambo bado yako vilevile. Serikali mpya ya Somalia lazima iweze kudumisha ulinzi kwa muda ili kuleta mabadiliko, walisema.
Abdi Yarre Hussein, mwenye miaka 47, ambaye alifika katika kambi za wakimbizi za Ifo mwezi Oktoba 2011, alisema kila wakati anapofikiria amani imerejea inaonyesha sio kweli.
Alisema alifanya kazi kama mfanyabiashara wa dhahabu na kuendesha ofisi inayoshughulika na ubadilishaji wa fedha nchini Somalia, lakini alipunguzwa kuvamia Kenya wakati usalama ulipozidi kuharibika. "Imekuwa ni kawaida; nilirejea Somalia kulipokuwa na utulivu na kuchukua nafasi ya Kenya wakati [Somalia] ikiwa na vurugu," Hussein aliiambia Sabahi.
Wageni wanaokuja kambini mara nyingi wanakuwa ni wanaotakia watu mema na ndugu kwa ajili ya chakula kwani wanasubiri kupewa kadi za wakimbizi zitakazowawezesha kupanga foleni kwa ajili ya kupata chakula na huduma za tiba zinazotolewa kambini, alisema.
"Tunaaibika kwa kiasi fulani lakini mazingira yametulazimisha sisi kujipanga katika foleni kwa ajili ya kupata misaada ya kibinadamu. Wengi kati yetu wanafanya biashara ambazo zinaweza kuhudumia familia za ndugu nyumbani. Tunachohitaji kwa sasa ni amani, ambayo imekuwa haipatikani kirahisi," alisema Hussein, baba mwenye watoto wanne.
Maisha yanaendelea
Kambi za wakimbizi mara nyingi zinatoa picha halisi ya mateso makali na kukata tamaa, lakini pia zinastawi kama kiungo cha kibiashara za bidhaa za petroli, magari ya mtumba na spea, vifaa vya umeme, nguo, madishi ya satelaiti na busta zake, simu za mkononi na vyakula.
"Badala ya kutafakari sana vita vilivyopita katika nchini yetu, maisha yanapaswa kuendelea alisema Adow Hussein Abdi, anayeendesha duka la dawa na maabara ya tiba katika kambi ya Hagadera.
Abdi, ambaye alikimbia Somalia mwaka 2000, aliiambia Sabahi kwamba baadhi ya wakimbizi wanaendesha taasisi za mafunzo. Kambi pia ina vyuo vya tiba, ambavyo wahitimu wake wanaendesha kliniki binafsi kambini. "Yote haya ni maandalizi ya wakati tutakapokuwa na amani nyumbani," alisema.
Wahitimu katika vyuo hivi vinavyoendeshwa na wakimbizi kwa mapenzi makubwa wanaitwa madaktari, walimu na wahandisi, alisema.
"Tunaweza kuwa tunakosa serikali yenye utulivu nyumbani, lakini hatukosi mawazo ya kibiashara. Ambapo kama kusingekuwa na vurugu nyumbani Somalia tungeiendeleza," alisema Abdi.
Chanzo sabahionline.com



No comments:
Post a Comment