ASHINDWA KUTETEA KITI MARA, AMPA ANGALIZO MSHINDI, TARIMBA ATAMBA DAR, WAMBURA ATUPWA
Waandishi Wetu
.jpg)
Makongoro Nyerere ameadhimisha vibaya kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha baba yake, Mwalimu Julius Nyerere baada ya kuangushwa kwenye uchaguzi wa kuwania Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara uliofanyika juzi na kumalizika usiku wa kuamkia jana.
Jana ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 13 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga yaliyokwenda sanjari na kuzimwa kwa Mwenge wa Uhuru.
Katika uchaguzi huo wa Mkoa wa Mara, Makongoro aliyekuwa akitetea kiti hicho, alipata kura 422 na kuzidiwa na mpinzani wake wa karibu, Christopher Sanya aliyepata kura 481 huku tisa zikiharibika.
Uchaguzi huo ilibidi urudiwe kwa kuwashindanisha wagombea wawili, kwani katika awamu ya kwanza wagombea wote hawakupata nusu ya kura kama kanuni za chama hicho zinavyotamka.
Awali, katika nafasi hiyo wagombea walikuwa watatu. Katika awamu ya kwanza, Sanya alipata kura 469, Makongoro (402) na mgombea mwingine, Enock Chambiri aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Mara alipata kura 144. Baada ya matokeo hayo ya awali, Chambiri aliondoka ukumbini hapo.
Matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa CCM Mkoa, yalitangazwa na Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Nazir Karamagi.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Makongoro alisema kuwa anakubaliana na matokeo hayo na kumuasa mshindi kufanya kazi kwa mujibu wa katiba. Pia alimtaka mshindi huyo kuvunja makundi aliyosema yameshamiri ndani ya chama hicho.
“Naomba uwe mwadilifu, Mkoa huu wa Mara ni mgumu sana kuufanyia kazi. Kazi ya uenyekiti siyo lelemama, hii ndiyo nafasi kubwa ambayo itatusaidia katika uchaguzi wa 2015.”
“Wewe ndiye kiongozi mkuu wa mkoa huu wa kupanga uongozi katika uchaguzi mkuu hivyo ukishindwa tutayumba, tunaomba utoe ushirikiano na ukemee hii dhambi ya kukata majina, kwani inaweza ikaingia kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa.”
Waliochaguliwa katika nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri ya Mkoa kupitia wilaya ni Josephat Seronga, Ester Nyarobi, Zuhura Makongoro, Jackson Waryoba, Josephat Kisusi na Felister Nyambaya.
Wengine ni Grace Bunyinyiga, Thabita Idd, Abdallah Jumapili, Kananda Kananda, Mariam Mkono na Samson Gesase.
Katika nafasi ya uenezi, Maximillian Ngesi amefanikiwa kutetea nafasi yake kama ilivyokuwa kwa Katibu wa Uchumi na Fedha, Marwa Mathayo.
Geita
Uchaguzi wa CCM mkoani Geita uliingia dosari baada ya karatasi za kupigia kura kupelea hali iliyosababisha kuahirishwa kwa uchaguzi huo kwa saa tatu. Hata hivyo, kasoro hizo zilirekebishwa na Joseph Msukuma kuibuka mshindi.
Awali, Msimamizi wa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema kuwa hakufurahishwa na utaratibu na kuagiza urudiwe upya.
Baada ya taratibu zote kukamilika, Lukuvi alimtangaza Msukuma mshindi kwa kupata kura 565 huku mpinzani wake, Jeremiah Mabula akipata kura 230 na John Chenge akiambulia kura tano.
Manyara
Diwani wa Kata ya Loiborsiret, wilayani Simanjiro, Manyara, Lucas Ole Mukusi amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika juzi mjini Babati, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho alisema Ole Mukusi alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 629.
Kificho alisema wagombea wengine wawili waliopitishwa kuwania nafasi hiyo walijitoa lakini walipigiwa kura na Godwin Nagol Kapurwa alipata kura 19 na Issa Omary Katuga alipata kura 18.
Alisema Fratey Massay alichaguliwa kuwa Katibu wa Siasa na Uenezi wa mkoa huo baada ya kupata kura 41 na kuwabwaga wagombea wengine, Michael Ngayda Tsaxara (kura tisa) na Ernest Fiita Sulle aliyepata kura mbili.
Nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa mkoa huo ilibidi irudiwe baada ya mshindi kutopata nusu ya kura baada ya Lucas Zacharia kupata kura 26, Gidamon Gapchojiga (14) na Janes Darabe kura tisa huku Gabriel Bukhay akiambulia kura tatu.
Uchaguzi huo uliporudiwa Kificho alimtangaza Zacharia ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Endiamtu, kuwa mshindi kwa kupata kura 34 dhidi ya Gapchojiga aliyepata kura 18.
Vicky Mushi (389) na Renalda Ndekubali (383) Babati Mjini, Wilaya ya Hanang’ ni Daniel Tluway (463) na Samwel Kawanga aliyepata kura 268.
Babati Vijijini washindi ni Mariam Kwimba (589) na Raphael Sumaye (273), Kiteto ni Sarah Losuritia (546) na Ahmed Muya (306) wakati Simanjiro ni Awadh Omary (360) na Paulo Sanka aliyepata kura 301. Wilaya ya Mbulu washindi ni Joseph Mandoo (353) na Aloyce Baira aliyepata kura 169.
Pwani
Mkoani Pwani, Mwinshehe Mlao ametetea nafasi yake ya Mwenyekiti wa Mkoa baada ya kupata kura 558 akiwashinda wapinzani wake, Seif Mpembenwe aliyepata kura 196 na Mziwanda Abubakari aliyeambulia na kura 13.
Walioshinda nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri ya Mkoa ni Mtumwa Kimbau (Mafia), Wilaya ya Mkuranga ni Haidani Ally na Ally Msakano, Kibaha Mjini ni Catherine Katele na Yusuph Mbonde na Bagamoyo ni Hafsa Kilingo na Imani Madega.
Walioshinda Kibaha Vijijini ni Fatuma Ngozi na Mwajuma Ndege huku Kisarawe wakiwa Asia Madina na Hassan Mavadana. Wilaya ya Rufiji washindi ni Hawa Mtopa na Bakari Mbonde.
Dar es Salaam
Mkoani Dar es Salaam, nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha imekwenda kwa Abbas Tarimba aliyepata kura 35 na kumshinda Eugen Mwaiposa aliyepata kura 12 wakati aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Richard Wambura akiambulia kura mbili.
Nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi ilikwenda tena kwa Juma Simba Gadafi baada ya kupata kura 40 na kuwabwaga wapinzani wake, William Malecela ambaye ni mtoto wa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mstaafu John Malecela aliyepata kura tisa na kada maarufu wa chama hicho, Salum Tambalizen aliyeambulia kura moja.
Imeandikwa na Anthony Mayunga na Ahmed Makongo (Musoma), Sanjito Msafiri (Kibaha), Jacqueline Masinde (Geita), Filbert Rweyemamu (Arusha), Bakari Kiango (Dar) na Joseph Lyimo (Babati).



No comments:
Post a Comment